DRFA yaziita mezani timu Dar

Muktasari:

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itashirikisha jumla ya timu 28 zimegawanywa kwenye vituo vinne Singida, Geita, Rukwa na Kilimanjaro

 

Dar es Salaam. Chama cha soka Dar es Salaam (DRFA), kimeziita mezani timu za hapa jijini zizoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa mwezi ujao ili kupanga  mikakati ya kuziwezesha kupanda Ligi Daraja la Pili msimu ujao.

Timu hizo tatu ambazo zitaiwakilisha Dar es Salaam kwenye mashindano hayo  yatakayofanyika kuanzia Mei Mosi hadi Mei 16, ni Karume Market, Ungindoni FC na Temeke Squad.

 Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu Kondo amesema nia ya chama hicho ni kuona jiji la Dar es Salaam linakuwa na idadi kubwa ya timu katika ligi kubwa za soka nchini hivyo kama mlezi wa klabu ni lazima wakutane nazo kupanga namna ya kutimiza lengo hilo.

  "Wengi wanaamini kwamba msaada siku zote huwa ni fedha kitu ambacho sio cha kweli. Unaweza ukawa ni ule wa ushauri na maoni kuhusiana na masuala ya kiufundi  na kiutendaji ili wasipate matatizo pindi wanapokwenda kwenye vituo  walivyopangiwa.

Huu ni utaratibu ambao tumeuweka kama chama na msimu ulioisha ulizaa matunda kwa timu ya Reha FC kufanikiwa kufuzu Ligi Daraja la Pili na huko ilifanya vizuri hadi kuweza kupanda Daraja la Kwanza," anasema Kondo.

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itashirikisha jumla ya timu 28 ambazo zimegawanywa kwenye vituo vinne ambavyo ni Singida, Geita, Rukwa na Kilimanjaro