Curry amfunika Lebron, Warriors mabingwa NBA

Muktasari:

  • Baada ya kubanwa mchezo uliopita, nyota Stephen Curry aliiongoza Warriors leo kwa kufunga vikapu 37, Ribaundi 6 na kusaidia vingine 4 katika ushindi wa vikapu 108-85 dhidi ya Cavaliers.

Dodoma. Golden State Warriors wametetea taji lao la ligi ya mpira wa Kikapu nchini Marekani NBA kwa ushindi wa jumla 4-0 dhidi ya wapinzani wao Clevaland Cavaliers alfajiri ya leo Jumamosi.
Baada ya kubanwa mchezo uliopita, nyota Stephen Curry aliiongoza Warriors leo kwa kufunga vikapu 37, Ribaundi 6 na kusaidia vingine 4 katika ushindi wa vikapu 108-85 dhidi ya Cavaliers.
Ushindi huo umewafanya Warriors kushinda taji la 3 ndani ya misimu 4 iliyopita ambapo wameshinda taji katika fainali bila kufungwa mchezo wowote tofauti na misimu iliyopita waliyocheza na Cavaliers.
Nyota LeBron James ameshindwa kuiongoza timu yake Cavaliers kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kihistoria kupindua matokeo ya 3-0 kwenye fainali ya mpira wa kikapu Marekani.
Hii ni mara ya pili Cavaliers kufungwa 4-0 kwenye fainali ambapo timu hiyo ndio ilikuwa ya mwisho kufungwa 4-0 kwenye fainali ya mwaka 2007 walipofungwa na San Antonio Spurs.