Conte ataja mahali anakotaka kwenda

Muktasari:

Mtaliano huyo anaweza kuachana na Chelsea mwishoni mwa msimu huu, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya mkataba wake aliosaini na miamba hiyo ya Stamford Bridge haujafika mwisho.

LONDON, ENGLAND

KOCHA Antonio Conte amesema kama ataondoka Chelsea basi ni kwa kazi moja tu, kwenda kuinoa timu ya taifa ya Italia na si vinginevyo.

Mtaliano huyo anaweza kuachana na Chelsea mwishoni mwa msimu huu, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya mkataba wake aliosaini na miamba hiyo ya Stamford Bridge haujafika mwisho.

Kwa siku za karibuni, Conte amekuwa akihusishwa na timu za PSG na Arsenal pia, kama akiondoka Stamford Bridge basi anaweza kuibukia kwenye timu hizo.

Lakini, ripoti zinadai Conte hana mpango wa kuachana na Chelsea na kama ikitokea ataondoka basi breki ya kwanza itakuwa Italia kukinoa kikosi cha Azzurri.

Mabosi wa Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) wamethibitisha mapema tu atamteua Conte aende akainoe timu ya taifa ya nchi hiyo kwa mara ya pili. Conte alipewa ofa hiyo mapema tu, lakini akagomea akidai anataka aendelee kubaki Chelsea.

Kutokana na hilo, PSG sasa wameanza kumfuatilia kwa karibu Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ili akakinoe kikosi chao msimu ujao.