Chuji afichua siri za Ndemla, Msuva

KIUNGO mwenye sifa ya kupiga pasi za rula, Athuman Idd ‘Chuji’ amemtaja kiungo wa Simba, Said Ndemla, kuwa ni zaidi ya viungo wote nchini kwa sasa, lakini akafichua mafanikio ya Simon Msuva anayetimkia El Jadida ya Morocco hayakuibuka tu kwani alipigika kinoma hadi kufikia alipo sasa.

Chuji anayepiga mazoezi kwa sasa ufukweni, uwanjani na kwenye Ndondo ili mradi tu ajihakikishie yuko fiti, hana timu baada ya kumaliza mkataba wake na KMC.

Chuji aliyetamba na zaidi na Yanga, alisema ubora wa Ndemla ni namna anavyofanya kazi yake uwanjani na anatofautiana na viungo wengine.

“Ndemla anajitambua, ana nidhamu, kipaji na mwili wa soka. Anacheza kiungo lakini anaweza kubadilisha matokeo muda wowote, sema tu ndiyo hivyo, kwa Tanzania ndiye mchezaji ninayemkubali na nimemchunguza kwa sababu ndiyo nafasi ninayocheza,” alisema Chuji.

Kuhusu Msuva alisema: “Katoka mbali na alikuwa anajua anachokitafuta, alikuwa anatoka uwanjani analia kutokana na zomea zomea ya mashabiki, lakini hakuwa mtu wa kukata tamaa alipambana na leo hii  anafurahi maisha, anakwenda zake Morocco.”