Chipukizi Mtanzania ajivunia kujifua La Masia ya Messi

Muktasari:

La Masia ni akademi ya FC Barcelona ambayo imewatoa wachezaji kadhaa wanaotamba kwenye kikosi cha timu hiyo akiwemo Lionel Messi anayeshikiria rekodi ya kutwaa tuzo tano za mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d'Or’.

Dar es Salaam. Mshambuliaji kinda wa Kitanzania, Adrian Kitare ametua nchini juzi  akitokea Hispania alipokuwa katika majaribio katika akademi ya La Masia.

La Masia ni akademi ya FC Barcelona ambayo imewatoa wachezaji kadhaa wanaotamba kwenye kikosi cha timu hiyo akiwemo Lionel Messi anayeshikiria rekodi ya kutwaa tuzo tano za mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d'Or’.

Akizungumzia majaribio hayo, Kitare alisema yamefungua njia kwake kwa kupata mawasiliano na mawakala wa soka ambao wameonekana kuvutiwa na kiwango chake.

“Nilitakiwa kufanya majaribio Marekani ambapo kuna kituo kidogo cha Barcelona, lakini nikakosa visa ila ukafanyika utaratibu  nikapata ya Hispania ambako walikubali niende ili watizame uwezo wangu,” alisema kinda huyo.

Hata hivyo Kitare alisema pamoja na kufanya kwake majaribio sio rahisi kupata nafasi ya moja kwa moja kujiunga na La Masia kutokana na umri wake kuwa juu ya miaka kati ya tisa hadi 11.

“Nina miaka 17, wao pale wanachukua vijana kuanzia miaka tisa hadi 11 na kwa sababu nilionyesha kiwango kizuri baadhi ya  mawakala walitoa mawasiliano yao,” alisema mshambuliaji huyo.