Chilunda mchezaji bora Ligi Kuu Mei

Muktasari:

  • Chilunda aliisaidia Azam FC,  akifunga mabao 6 kwa mwezi huo, ambapo kati ya mabao hayo matatu ‘hat trick’ alifunga katika mchezo mmoja.

Dar es Salaam. Mchezaji wa Azam FC, Shaaban Idd Chilunda amechaguliwa kuwa mchezaji Bora wa Mei wa Ligi Kuu ya VPL, baada ya kuwashinda wenzake wawili, Jacob Massawe wa Ndanda na Edward Shija wa Kagera Sugar.


Chilunda aliisaidia Azam FC,  akifunga mabao 6 kwa mwezi huo, ambapo kati ya mabao hayo matatu ‘hat trick’ alifunga katika mchezo mmoja.


Chilunda atazawadiwa tuzo, king'amuzi cha Azam na fedha taslimu Sh.1 milioni kutoka kwa wadhamini Vodacom.


Kwa mwezi huo Azam ilicheza michezo minne na kupata pointi tisa, baada ya kushinda michezo mitatu na kufungwa mmoja ikibaki katika nafasi yake ya pili na hakuwa na kadi yoyote.


Kwa upande wa Shija aliisaidia Kagera Sugar kupata pointi 10, akifunga mabao matatu katika michezo minne iliyocheza na timu  hiyo.


Massawe aliisaidia timu yake isishuke daraja ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu, akiisaidia kushinda mechi mbili kati ya nne walizocheza na hivyo kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 15hadi ya 14 .