Chilunda, Farid kuwasha moto Hispania

NYOTA wa Kitanzania, Shaaban Idd  Chilunda  amejiunga na Farid Mussa kuanza maisha yake  mapya ya soka  nchini Hispania kwenye klabu ya CD Tenerife itakayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo ambayo ni maarufu kama Segunda.

Chilunda ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kagame akiwa na Azam, alitua Hispania Agosti  10 na moja kwa moja kuandaliwa hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hatusa Red Volkswagen Canarias kwa ajili ya utambulisho wake.

Chilunda amejiunga na CD Tenerife kwa kusaini mkataba wa mkopo wa miaka miwili  na mara baada ya kutambulishwa siku iliyofuata akaanza mazoezi yake ya kwanza mchana kwenye kituo cha Ciudad Deportiva Javier Perez.

Akiwa na furaha nchini humo, Chilunda alisema ametua Tenerife kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye msimu mpya wa Segunda na alienda mbali kwa kusema mbali na kufunga atashirikiana vyema na wachezaji wenzake kwa kutengeneza nafasi za mabao.

“Nilikuwa mwenye furaha kubwa tangu niliposikia CD Tenerife wananitaka nijiunge nao.Nitacheza kwa nguvu na kwa kiwango kizuri, hilo siyo tatizo kwangu, japokuwa najua Hispania itakuwa tofauti, ila nitazoea kwa haraka.

"Faridi   ni mfano mzuri kwangu, ninavyomuana anacheza sasa ni tofauti ilivyokuwa kabla," alisema Chilunda ambaye ni zao la akademi ya Azam ambalo lililelewa na kupandishwa kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, Mkurungezi wa ufundi wa CD Tenerife, Alfonso Serrano naye ametia neon  kwa kusema  Chilunda  ambaye yupo hapo kwa mkopo wa miaka miwili akionyesha kiwango cha juu basi watamnunua moja kwa moja.