Chelsea yafanya maangamizi England

Muktasari:

Pazia la Ligi Kuu England limefunguliwa rasmi jana kwa timu mbalimbali kuanza kampeni ya kusaka ubingwa

London, England. Kocha Maurizio Sarri ameanza vizuri kibarua chake katika Ligi Kuu England wakati Chelsea ikipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Huddersfield Town. Sarri ambaye amekuwa kocha wa 10 katika kipindi cha miaka 10, baada ya kuchukua mikoba ya Antonio Conte msimu huu alishudia kikosi chake kitawala mchezo huo tangu mwanzo hadi mwisho.

Chelsea ilipata bao la kuongoza dakika 34, lililofungwa na N'Golo Kante akimalizia vizuri krosi ya Willian iliyompita kipa Huddersfield, Ben Hamer.

Kiungo Jorginho aliyemfuata Sarri kutoka Napoli kuja Chelsea msimu huu alifunga bao lake la kwanza kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na beki wa Christopher Schindler kumchezea vibaya Marcos Alonso.

Pedro alikamilisha kalamu hiyo kwa kufunga bao la tatu kwa Chelsea kwa ustadi mkubwa.

Katika michezo mingine iliyochezwa leo Fulham ikiwa nyumbali ilikubali kipigo cha mabao 0-2 kutoka Crystal Palace shukrani kwa magoli ya Schlupp, Zaha.

Bournemouth ilitumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kuichapa Cardiff mabao 2-0 yaliyofungwa na Fraser na Wilson). Mabao mawili ya Pereyra yalitosha kuipa Watford ushindi wa 2-0 dhidi ya Brighton, wakati mapema Tottenham ilishinda 2-1 dhidi ya Newcastle.