Cheki Mbongo alivyopania kumfuata Ronaldo Serie A

Muktasari:

  • Bale, anayeichezea pia Timu ya Taifa ya Wales, alikuwa na ndoto za kuwa mwanasoka wa kulipwa, lakini hakuwazia kama atafikia kiwango cha kuitetemesha dunia kama afanyavyo sasa.

GARETH Bale. Ndio ni Bale, kwa sasa ni miongoni mwa mastaa wakubwa wa soka duniani akifanya yake kikosini kwa wababe wa Hispania, Real Madrid huku akitajwa kuitoa udenda Manchester United.

Bale, anayeichezea pia Timu ya Taifa ya Wales, alikuwa na ndoto za kuwa mwanasoka wa kulipwa, lakini hakuwazia kama atafikia kiwango cha kuitetemesha dunia kama afanyavyo sasa.

Alitumia muda wake mwingi kumtizama Ronaldo de Lima wa Brazil na alitamani japo afikie nusu ya uwezo wake. Kila alipocheza na watoto wenzake enzi hizo, alikua akijiita Ronaldo japo hakufikiri anaweza kuwa mahiri.

Jinsi alivyokuwa akifikiria Bale ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 28 na aliye mpwa wa mchezaji wa zamani wa Cardiff City, Chris Pike ni tofauti na ilivyo kwa mshambuliaji wa Kitanzania, Zakaria Kibona, anayecheza soka la kulipwa Finland.

Kibona aliyezaliwa Machi 14, 1990 jijini Dar es Salaam, anaichezea IF Gnistan ya Daraja la Kwanza huko Finland walikotokea mastaa kama vile, Niklas Moisander wa Werder Bremen na Perparim Hetemaj wa Chievo.

Mshambuliaji huyo, anasema pamoja na ndoto aliyokuwa nayo ya kucheza soka la kulipwa, lakini yeye amepania kuwa mchezaji wa daraja la juu atakayetingisha kwenye ligi kubwa Ulaya.

“Nimedhamiria hilo na ndio maana unaona niliamua kuanzia harakati zangu huku (Ulaya). Unajua nimekuwa nikisikia kuwa nyumbani Tanzania ni vigumu kupata nafasi kwa haraka ya kucheza soka la kulipwa,” alisema.

“Kuna jamaa zangu wanasema Bongo unaweza kuwa na kipaji lakini kukawa na mlolongo mrefu wa kupata nafasi, ni tofauti na ilivyo huku (Ulaya) kwani uwezo wa mchezaji ndio unaoamua na sio mambo mengine.

“Ligi ya Italia ni chaguo langu la kwanza kama itatokea nafasi ya kucheza soka kwenye mataifa mengine makubwa, lakini haina maana nisipopata nafasi huko kuwa siwezi kwenda kwingine.”

Kibona mwenye mabao matatu ndani ya michezo tisa klabuni kwake, ameongeza kuwa yupo tayari muda wowote kutua Tanzania kwa ajili ya kuichezea Taifa Stars.

Mshambuliaji anafichua nia ya kuichezea Stars amekuwa nayo tangu mwaka 2008 alipoanza rasmi kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Atlantis.

“Mwaka 2009 niliingia kwenye utata wa viongozi wa soka wa Finland ambao walihitaji kunitumia kwenye timu yao ya taifa, lakini nilikataa kwa sababu nilijiona naweza kuwa msaliti kwa taifa langu la Tanzania,” alisema.

“Sijaitwa bado Stars, lakini naamini ipo siku nitatambulika uwezo wangu. Hata kama nitakosa nafasi ya kuchezea Taifa Stars, nipo tayari nimalize soka langu bila ya kucheza kwenye timu yoyote ya taifa, kikubwa nikipata nafasi kwa sasa ni kuisaidia Gnistan kupanda daraja ili msimu ujao tushiriki Ligi Kuu Italia,” anasema Kibona.

Kama watafanikiwa, basi kuna uwezekano akapambana na staa wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ambaye sasa ameondoka Real Madrid na kujiunga na Juventus ya Italia.

Akizungumzia mafanikio makubwa ambayo amewahi kuyapata kwenye uchezaji wake soka akiwa Italia, Kibona anasema ni kuchukua ubingwa wa ligi ya vijana wakati akiwa Atlantis.

Mshambuliaji huyo alianzia soka lake kwenye timu hiyo na baadaye akapandishwa na kucheza kikosi cha kwanza kwa miaka miwili, 2008 na 2009.

Baada ya kufanya vizuri miaka hiyo, Kibona alitua Helsingin Jalkapalloklubi ambayo aliichezea nusu mwaka kisha akajiunga na Klubi-04 kwa mkataba wa miezi sita na mara baada ya kumalizika akapokea ofa ya kujiunga na PK-35 Vantaa.

Akiwa klabuni humo, Kibona alicheza mechi 23 na kufunga mabao sita kisha akitimkia Malta ambako alipata dili la kujiunga na Mosta FC ya Ligi Kuu.

Kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Mosta kulimfanya kutoongeza mkataba mwishoni mwa msimu wa 2011/ 12.

Kibona anadai kilichomkwamisha kung’ara kwenye ligi akiwa na Malta ni utofauti wa mazingira uliomfanya kuumwa mara kwa mara na mwisho wa siku kuishia kucheza mechi tatu tu msimu mzima.

“Huwezi kuamini, sikufunga hata bao la kuotea kule Malta,” anasema huku akicheka mshambuliaji huyo ambaye anaukubali uwezo wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Aliporejea Finland, Kibona alizichezea klabu za madaraja tofauti kama vile HIFK, Viikingit, BK-46 na Legirus Inter kabla ya mwaka 2017 ambapo alijiunga na timu yake ya sasa.