Cheka apigwa TKO Poland

Muktasari:

  • Cheka hajawahi kushinda pambano lolote alilocheza Ulaya katika miaka zaidi ya mitano iliyopita

Dar es Salaam. Bondia Francis Cheka usiku wa kuamkia leo Jumapili  amechezea kipigo cha Technical Knock Out (TKO) kutoka kwa bondia Dariusz Sek nchini poland.

Cheka amepigwa raundi ya tatu ya pambano lililokuwa la raundi nane la uzani wa juu mwepesi dhidi ya Sek.

Mtanzania huyo alicheza dakika nane tu kabla ya kukubali kipigo hicho kwenye ukumbi wa Kopalnia Soli huko Wieliczka.

Katika pambano hilo Cheka alicheza hadi raundi ya tatu kabla ya  refarii Robert Gortat alimtangaza Sek kuwa mshindi kwa matokeo ya TKO.

Katika hatua nyingine, mabondia Abdallah Pazi 'Dulla Mbabe' na Twaha Kiduku wamemaliza pambano lao kwa sare baada ya majaji kutoa matokeo ya sare kwenye pambano lililofanyika Dar es Salaam.

Majaji,  Aghapeter Mnazareti alitoa pointi 97-93 kwa Kiduku, Said Chaku alitoa pointi 95-95 na Ibrahim Kamwe (Big right) alitoa pointi 95-95 matokeo ambayo yalishindwa kuamua nani mbabe kati yao.