Chamberlain ndio basi tena Kombe la Dunia

Muktasari:

Chamberlain aliumia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati klabu yake ya Liverpool ilipovaana na AS Roma kwenye nusu fainali ya kwanza uwanjani Anfield.

NI pigo kubwa kwa timu ya Taifa ya England, baada ya vipimo kuonyesha kuwa kiungo wake Alex Oxlade-Chamberlain, ameumia na atalazimika kuwa nje ya muda mrefu. Kwa hatua hiyo kiungo huyo hatakuwemo kwenye kikosi kitakachoshiriki Kombe la Dunia kule Russia.
Chamberlain aliumia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati klabu yake ya Liverpool ilipovaana na AS Roma kwenye nusu fainali ya kwanza uwanjani Anfield.
Taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita, imeonyesha kuwa Chamberlain ataikosa michuano hiyo mikubwa itakayofanyika nchini Russia kuanzia mwezi Juni.
Tayari timu ya madaktari wa Liverpool wamemweleza kocha wa England, Gareth Southgate kuwa, Chamberlain atakuwa nje kwa muda mrefu.
Kuumia kwake ni kama gundu kwani, wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 hakuwemo kwenye kikosi cha England kule Brazil kutokana na kuwa majeruhi. Pia, mwaka 2016 alikosa fainali za Mataifa Ulaya kutokana na kukabiliwa na maumivu ya enka na sasa, kipute cha kule Russia atakiangalia kwenye luninga tu.