Chama la Kanda ya Ziwa ni balaa

WAKATI Ligi Kuu ikielekea ukingoni, tayari timu za Kanda ya Ziwa zimeshajihakikishia kucheza tena Ligi hiyo msimu ujao baada ya kufikisha pointi ambazo zinatosha kuzibakisha ndani ya Ligi Kuu.

Kanda ya Ziwa kwa sasa inawakilishwa na timu nne ambazo muda mwingi msimu huu zilitumia katika eneo la kushuka daraja kabla ya kujiweka salama dakika za mwisho. Timu kutoka ukanda huu ni Kagera Sugar, Stand United, Mwadui FC na Mbao, ambapo kwa msimu ujao zitaongezeka kufikia tano baada ya Alliance FC kupanda daraja.

Licha ya timu hizo kupitia wakati mgumu,l akini zimejitahidi na kila moja imeweza kuwajibika kwa nafasi yake ili kuhakikisha inakwepa janga la kushuka daraja.

Kutokana na uwezo ulioonyeshwa na timu hizo, Mwanaspoti limeandaa kikosi cha wachezaji 11 na makocha ambao wameonekana kuwa bora hadi sasa kwenye timu zao.

Juma Kaseja-Kagera

Kipa huyu mkongwe nchini ndiye ameonekana kuwa bora kwenye klabu za Kanda wa Ziwa kutokana na kuwa namba moja kwenye kikosi hicho.

Kaseja aliyewahi kutamba na timu za Simba, Yanga na Taifa Stars ameonyesha uwezo na uzoefu wake na kuifanya Kagera Sugar kufungwa idadi ndogo ya mabao ukilinganisha na timu nyingine kutoka ukanda huu.

Pia, nidhamu kujituma na kutokata tamaa vimeendelea kumbeba mkongwe huyu kwani licha ya timu yake kupitia wakati mgumu wa kutopata matokeo mazuri mwanzoni mwa ligi, bado aliendelea kuvumilia.

Katika kuonyesha uwezo wake zaidi, hivi majuzi alichomoa penalti ya Emanuel Okwi wakati Simba ikiloa bao 1-0 wakati ikikabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Boniface Maganga-Mbao

Nyota huyu chipukizi anayekipiga Mbao FC, anaingia kwenye kikosi hiki kutokana na uwezo alioonyesha akiwa na timu yake kwani ameisaidia kwa kiasi kikubwa.

Maganga amekuwa akijumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa nyakati tofauti, ameonekana kuimudu nafasi hii ya iliinzi licha ya muda mwingine kucheza nafasi hata za mbele kulingana na mipango ya kocha na mchezo husika.

David Luhende-Mwadui

Hakuna asiyemjua beki huyu wa kushoto wa Mwadui FC, kwani kiwango chake kimekuwa cha juu tangu amejiunga na timu hiyo mpaka sasa. Luhende amekuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Mwadui kwa msimu mzima.

Beki huyo amekuwa kwenye kiwango bora tangu akiwa Yanga huku akiendelea kuwashawishi makocha mbalimbali wanaotua klabuni humo kumpanga.

Iddy Moby-Mwadui

Beki huyu wa Mwadui FC naye anaingia kwenye kikosi hiki kutokana na ufundi wake uwanjani na ameweza kudumu kwenye timu hiyo kwa takribani misimu mitatu na kiwango chake kimekuwa cha juu kwa muda wote.

Moby ni miongongi mwa mabeki bora wa kati ndani ya Ligi Kuu, akicheza karibu mechi zote za Mwadui kwa msimu huu. Uwezo wake mkubwa wa kucheza mipira ya juu na chini pamoja na utulivu wake vimekuwa msingi wa safu ya ulinzi ya Mwadui.

Yusuph Ndikumana-Mbao

Beki huyu wa kati anayekipiga Mbao FC hakuna asiyejua shughuli yake uwanjani. Amekuwa nahodha tangu alipotua klabuni hapo miaka miwili iliyopita.

Ndikumana raia wa Burundi amekuwa na mwendelezo mzuri katika kazi yake ya soka na hadi sasa anamezewa mate na klabu za Simba, Yanga na Azam kutokana na uwezo wake.

Nahodha huyo amekuwa mhimili wa safu ya ulinzi ya Mbao na chaguo namba moja kuanzia kwa Uongozi, Benchi la Ufundi na hata wadau na mashabiki wanamuelewa kazi yake.

Awadh Juma-Mwadui

Kiungo huyu licha ya kukosa namba kwenye timu yake ya Simba msimu uliopita na kujiunga na Mwadui, msimu huu amekuwa mchezaji aliyeisaidia kwa kiasi kikubwa timu hiyo.

Kutokana na umuhimu wake, benchi la ufundi lilimvisha kitambaa cha unahodha kuhakikisha anawapanga wenzake ili kuiweka timu nafasi nzuri.

Utulivu wake uwanjani, nidhamu na kujituma ni moja ya mambo yanyompa sifa nyota huyu na kuingia kwenye ‘First Eleven’ ya timu ya Kanda ya Ziwa ambayo ikikaa pamoja inaweza kufanya kweli.

Japhet Makalai-Kagera Sugar

Winga huyu wa Kagera Sugar amekuwa mchezaji mwenye uwezo kikosini na ameisaidia timu yake kuepuka rungu la kushuka daraja msimu huu.

Amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Kagera, akiifungia timu hiyo mabao matano na kutengeneza mengine kadhaa ikiwemo dhidi ya Simba ambapo alimpigia krosi safi Edward Christopher aliyefunga.

Abdallah Seseme-Mwadui

Kiungo huyu anayekipiga Mwadui bado anaendelea kutesa na kiwango chake hakijashuka tangu akiwa Simba na Toto Africa. Utulivu na nidhamu yake uwanjani vimekuwa ngao kubwa kwake.

Kasi yake uwanjani na uwezo wa kuzifumani nyavu na kutengeneza mabao bado inampa nafasi ya kuaminiwa na Kocha Ally Bizimungu pamoja wachezaji wenzake.

Seseme ameweka rekodi kadhaa msimu huu ikiwemo ya kufunga bao la mapema zaidi dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani. Alifunga bao hilo katika sekunde ya 12.

Paul Nonga

Nahodha huyu msaidizi wa Mwadui naye yumo kwenye kikosi hiki kutokana na uwezo wake aliounyesha kwa msimu huu, ameisaidia timu yake kuifungia mabao manane hadi sasa.

Uwezo wake binafsi wa kumiliki mpira, kushambulia na kupiga chenga za maudhi vinambeba straika huyu wa zamani wa Yanga, Mbeya City na JKT Oljoro.

Habib Kyombo-Mbao

Kwa kiwango anachoonyesha chipukizi huyu wa Mbao hadi sasa kinamfanya kuwa straika hatari zaidi kutoka ukanda huu.

Mbinu yake ya ufungaji mabao aliyonayo hadi kufikia hatua ya kumezewa mate na klabu kubwa nchini unamuweka kwenye kikosi cha Kanda ya Ziwa bila ubishi. Kyombo amefunga mabao tisa Ligi Kuu mpaka sasa.

Jafary Kibaya

Mshambuliaji huyu wa Kagera Sugar ndiye anahitimisha kikosi hiki kutokana na mchango wake ndani ya timu hiyo iliyoepuka kikombe cha kushuka daraja dakika za mwisho.

Kibaya ameifungia pia Kagera Sugar mabao sita na amekuwa msaada mkubwa katika kutengeneza nafasi za mabao, huku akionekana kuwa uwezo binafsi uwanjani.