Celtic yashikwa, Benfica yapeta Ligi ya Mabingwa

London, England. Licha ya kucheza nyumbani na kujipatia bao la mapema lililofungwa na McGregor dakika ya 17, bado Celtic ya Scotland ililazimishwa sare ya bao 1-1 na AEK Athens ya Ugiriki.

Celtic ilishindwa kabisa kutumia mwanya wa upungufu kutokana na  AEK Athens iliyocheza kwa kipindi kirefu cha pili ikiwa na wachezaji kumi kutokana na Konstantinis Galanopoulos kulimwa kadi nyekundu baada ya kadi mbikli za njano.

Katika kipindi cha pili AEK Athens, ilipambana vilivyo na kufanikiwa kusawazisha bao likifungwa Viktor Klonaridis kwa mkwaju wa mbali.

Timu hizo zitarudiana Jumanne ya wiki ijayo ili kumpata mshindi atakayetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Matokeo mengine ya mchezo huo yalishuhudiwa timu ya RB Salzburg ikiutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani ikiichapa kwa mabao 3 -0 Shkendija FC, nayo PAOK Salonika ya Ugiriki iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Spartak Moscow ya Russia.

Mechi nyingine za Ligi hiyo zilitarajiwa kuchezwa Jumanne na matokeo yalikuwa Dynamo Kiev na Slavia Prague zilitoka sare ya bao 1-1, BATE Borisov nayo ikichapa bao 1-0 FK Qarabag.

Timu ya Spartak Moscow ilishindwa kuwika nyumbani baada ya kufungwa mabao 3-2 na PAOK Salonika, Dinamo Zagreb ya Ukraine ilichapa FC Astana mabao 2-0 na Fenerbahçe ya Uturuki ikachapwa kwa bao 1-0 na Benfica ya Ureno.

Aidha timu ya MOL Vidi na Malmö FF zilitoka sare ya bao 1-1, Shkendija ikachapwa mabao 3-0 na FC Red Bull Salzburg, Ajax Amsterdam ya Uholanzi ikabanwa na Standard Liege ya Ubelgiji, Spartak Trnava ikatoka sare ya bao 1-1 na Red Star Belgrade.