Cecafa yaifungia Gor Mahia miaka miwili, Kerr aonywa

Muktasari:

Siyo mara ya kwanza kwa Gor Mahia kukataa kuvaa medali zao, kwani Februari 2016, waligoma kupokea zawadi ya mshindi wa pili

Nairobi. Shirikisho la Vyama vya Soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), imeifungia klabu ya Gor Mahia, kutoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame kwa miaka miwili kwa kosa la utovu wa nidhamu, huku kocha wao, Dylan Kerr akipewa onyo kali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Cecafa iliyoifikia Mwanaspoti Digital, kupitia kwa Katibu wake Mkuu, Nicholas Musonye ni kwamba, Mabingwa hao wa soka nchini walionesha utovu wa nidhamu katika makala ya mwaka huu ya mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika jan nchini Tanzania, huku Azam wakifanikiwa kutetea taji lao.

Hatua ya kamati ya Cecafa, imekuja baada ya kupitia tipoti ya makamisaa wa michezo ya mabingwa hao mara 16 wa soka nchini, iliyoonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kitendo cha Kogalo kugoma kuvalishwa medali za shaba kama washindi wa tatu hapo jana.

Sio hilo tu, Kamati hiyo ilisena kuwa sababu za kuifungia Gor Mahia ni kitendo cha kugoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo walizopangiwa kwa madai ya imani za kishirikina, pamoja na dharau wa Kocha wao dhidi ya waamuzi wa mashindano hayo.

Aidha, Musonye amemuonya Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr, akimtaka kuwaheshimu waamuzi. Alisema Kerr alionesha kuwadharau waamuzi katika michuano hiyo iliyomalizika jana Jijini Dar es Salaam, huku akifichua kuwa Kogalo hawatapewa shilingi milioni moja, ambazo ni zawadi kwa mshindi wa tatu.

"Tumeamua kuifungia Gor Mahia, hawatoruhusiwa kushiriki michuano hii kwa kipindi cha miaka miwili. Waligoma kuvaa medali bila sababu, Kocha wao anawadharau waamuzi na pia hapo kabla waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia, hiyo ni dharau," alisema Musonye.

Itakumbukwa kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Gor Mahia kukataa kuvaa medali zao, kwani Februari 2016, waligoma kupokea zawadi ya mshindi wa pili, walipopigwa na Bandari 1-0, katika mchezo wa Super Cup, ambapo wao waliingia wakiwa mabingwa watetezi wa KPL huku Bandari wakiwa ni mabingwa wa Ngao ya jamii.