Cannavaro sasa amsuka mrithi wake

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Cannavaro alisema anaamini uwepo wa wakongwe Kelvin Yondani aliyerithishwa cheo chake cha unahodha pamoja na Andrew Vincent ‘Dante’, ukuta wa timu hiyo upo salama, lakini mrithi wake halisi ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

MENEJA mpya wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amekiangalia kikosi chao na kuwataja mabeki watatu wanaoweza kuchukua nafasi yake, lakini akamtaja pia anayeamini kama akitulia atakuwa mrithi wake halisi huku akijipa jukumu zito juu yake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Cannavaro alisema anaamini uwepo wa wakongwe Kelvin Yondani aliyerithishwa cheo chake cha unahodha pamoja na Andrew Vincent ‘Dante’, ukuta wa timu hiyo upo salama, lakini mrithi wake halisi ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Cannavaro alisema Ninja ni beki anayeweza kurithi mikoba yake na kwamba tayari ameshaanza kazi ya kumsuka ili awe bora kama yeye.

Beki huyo alisema mambo mawili ambayo anataka kuyasuka kwa Ninja ni kumfanya anapokaribia kumkaba mshambuliaji aweze kuchelewa kidogo katika kumsoma ili asiwe anasababisha ‘faulo’ nyingi.

Meneja huyo alisema jambo la pili ni kumbadili Ninja ili asiwe anapenda kufanya ‘faulo’ dhidi ya mshambuliaji aliyegeukia lango la wapinzani makosa, ambayo ni rahisi kupewa kadi.

Mkongwe huyo ambaye mechi ya kwanza kati ya zitakazofanyika kumuaga rasmi itachezwa kesho, alisema jingine analotaka kumsuka Ninja ni kuboresha uwezo wake wa kuruka vichwa ili uwe na faida ya kuifungia mabao timu hiyo.

“Kuna mambo nimeanza kumsuka ili awe bora zaidi na kuna makosa ambayo anatakiwa kuyaondoa. Ninazungumza naye ili aweze kubadilika na mpaka sasa naona ameanza kushika na kuyafanyia kazi,” alisema.