VIDEO: Cannavaro: Hatuachi kitu Singida

Singida.Yanga imewasili mkoani Singida kimyakimya kuikabiri Singida United, bila ya kupata mapokezi makubwa kutoka kwa  mashabiki wake kama ilivyozoeleka inapokuwa inaingia mikoani kucheza mechi za mashindano mbalimbali.

Yanga iliondoka leo asubuhi mkoani Morogoro kuelekea Singida tayari kwa mchezo wao wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya wenyeji wao, Singida United itakayochezwa Aprili Mosi kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikiwa itapoteza mechi hiyo ya Robo Fainali ya Kombe la FA, nafasi pekee kwake kushiriki mashindano ya kimataifa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu vinginevyo italazimika kusubiri hadi mwaka 2020.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub (Canavaro) alisema kikosi chao kipo tayari kupambana na Singida United kupigana hadi tone la mwisho katika mchezo wa robo fainali ya kombe la FA ili kupata matokeo mazuri yatayosaidia kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Canavaro alisema kuwa wachezaji wenzake kwa sasa wameelekeza akili katika mchezo dhidi ya Singida United ili kupata matokeo mazuri yatayosaidia kusonga mbele.

Canavaro amesema kuwa wachezaji wana morali dhidi ya mchezo huo ili kutengeneza njia nzuri ya kushiriki michuano ya kimatifa katika msimu ujao.

“Tunaiheshimu Singida United ni timu nzuri na tunategemea kupata ushindani mkubwa kutoka kwao lakini tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na lengo letu ni kupata ushindi kwenye uwanja wa Namfua ili kutengeneza njia ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.”alisema Cannavaro.

Cannavaro alisema kambi ya Morogoro, wachezaji wameifurahia kutokana na mandhari nzuri na hewa safi.

Cannavaro alisema mchezo huo utakuwa na ushindani kutokana na kila timu kuwa na wachezaji wenye vipaji lakini yoyote atayechanga vizuri karata ndiye atayeshinda huku akiwaomba mashabiki wa klabu ya Yanga kuwaombea dua njemma ili kuweza kushinda mchezo huo.