CAF yaisogezea Yanga mamilioni

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina

KAMA kweli Yanga inayataka mamilioni ya fedha za CAF, huu ndio wakati wake kwani usiku wa jana, Shirikisho hilo la Soka Afrika, liliwapangia wawakilishi hao pekee wa Tanzania Wahabeshi, Welayta Dicha kutoka Ethiopia katika Kombe la Shirikisho.

Yanga iliyokwama kuvuna Sh1.3 bilioni za Ligi ya Mabingwa Afrika, imepangwa kuvaana na Dicha iliyotolewa jasho na Zimamoto ya Zanzibar kabla ya kuwakomalia Zamalek ya Misri na kuwatoa kwa mikwaju ya penalti katika droo iliyofanyika Cairo.

Dicha iliyoasisiwa mwaka 2009 inashiriki michuano hiyo ya Afrika kwa mara ya kwanza na kama Yanga itaamua kukomaa nao kwenye mchezo wa kwanza utakaopigwa kati ya Aprili 6-8, basi Sh600 milioni za kutinga makundi zitawahusu.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina aliliambia Mwanaspoti jana baada ya droo kuwa, licha ya kwamba hajawahi kukutana na timu hiyo, lakini analijua soka la Ethiopia na pia atatafuta video za timu hiyo ili kuwasoma kabla ya kumalizana nao mwezi ujao.

Lwandamina alisema vijana wake kuanzia leo Alhamisi wataanza tizi kwa ajili ya mechi hiyo na ile ya robo fainali ya Kombe la FA, huku akijua kuwa wapinzani wao sio wa kubezwa kama waliweza kuing’oa Zamalek moja ya vigogo vya soka Afrika.

“Sijawahi kukutana na Dicha, lakini naijua St George , hivyo kwa sasa tutafanya kila njia kuipeleleza inacheza soka la aina gani, ili tuweze kupata matokeo mazuri nyumbani. Hakuna njia ya mkato katika michuano hii, ila kujipanga lichja ya kwamba tutawakosa mastaa wetu kadhaa kutokana na kutumikia kadi za njano,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa alisema wanasubiri benchi la ufundi kuwaambia wanataka nini ili kuelekea kwenye mchezo huo, lakini kiu yao ni kuona wanasonga mbele na kuchjeza makundi ya Shirikisho kwa mara ya pili.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema katika hatua ambayo wamefikia hakuna timu ndogo na hawatawadharau wapinzani wao kwa kuwa hawana jina kubwa katika historia ya soka na kama wamefika hapo basi ni timu ambayo inauwezo.

“Tumeipokea droo na tushafahamu tunaanza na timu gani kwahiyo maandalizi yanaanza sasa na kubwa ambalo tutalifanya ni kutofanya makosa ambayo tumeyafanya katika michuano ambayo tumetolewa ili kosonga mbele katika hatua hii,” alisema Saleh.

Yanga iliwahi kung’olewa na Dedebit katika michuano ya CAF mwaka 2011 kwa jumla ya mabao 4-2, ikitoka sare ya 2-2 nyumbani kabla ya kulala 2-0 ugenini. Hivyo haipaswi kuwachukulia poa wapinzani wao hao wanaoshika nafasi ya nane katika msimamko wa Ligi Kuu ya nchini kwao inayoongoza na Dedebit kwa alama 29.

WELAYTA DICHA

Wapinzani hao wa Yanga ni wageni kwenye mashindano hayo ya kimataifa, ikiwa huu ndio msimu wao wa kwanza kushiriki michuano ya Afrika na kutinga japo sio ya kubeza kwani baada ya kutoka sare ya 1-1 na Zimamoto kabla ya kushinda nyumbani bao 1-0 katika mechi za raundi ya kwanza iliitoa Zamalek. Iliifunga Zamalek mabao 2-1 nyumbani kabla ya kulala ugenini 2-1 na kupigiana penalti na kushinda 4-3. Nyota pekee kwenye kikosi hicho ambaye amesalia mpaka leo tangu kuanzishwa 2009 ni Mubarek Shikur aliyeiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wao wa kwanza kwenye ligi ya Ethiopia, 2017.