CAF: Ruksa kutumia Kasarani mechi ya USM Algiers

Thursday May 10 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Sasa ni rasmi kuwa, mashabiki wapatao 60,000 watapata fursa ya kushuhudia mechi ya kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika, kati ya Gor Mahia dhidi ya USM Algiers ya Algeria, utakaopigwa Mei 16, mwaka huu, jijini Nairobi.

Hii ni baada ya shirikisho la soka barani Afrika CAF, kuridhika na hali ya uwanja wa Kasarani, ambao ulikuwa umefungwa kwa takribani miezi minne, kupisha marekebisho.

Awali CAF, ilikuwa imeridhia uwanja wa Kenyatta, mjini Machakos utumike kwa ajili mtanange huo, lakini baada ya kuridhika mwenendo wa zoezi la ukarabati wa uwanja wa Kasarani, shirikisho hilo, limepitisha uwanja huo kutumika kwa ajili ya mechi hiyo.

Hii ni habari njema kwa wapenzi wa soka nchini, pamoja na mashabiki wa Kogalo, kwani kupeleka mechi hiyo Machakos ingepelekea mashabiki kushindwa kuishangilia timu yao, kutokana na umbali lakini pia kutokana na udogo wa uwanja wenyewe. Uwanja wa machakos unachukua watazamaji wapatao 10,000 tu.

Mabingwa hao mara 16 wa soka nchini, wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo na pointing yao moja baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Rayon Sports (Rwanda). Kwa upande wao, USM Algiers wanaongoza kundi wakiwa na pointi tatu, baada ya kuitandika Yanga (Tanzania) 4-0.

Wakati huohuo, kikosi cha Kogalo kitashuka dimbani kuwakabili Hull City ya England, kwenye dimba la Kasarani, katika mechi ya kirafiki iliyopewa jina la Hull City Challenge, kuanzia saa 9 mchana.

Kogalo walipata fursa ya kukipiga na Hull City baada ya kuwafunga AFC Leopards, kwa matuta, mjini Nakuru.