Bushiri ataka mpango wa kuinua soka la Z’bar

Zanzibar. KOCHA wa Mwembeladu, Ali Bushiri amesema pamoja na kuwepo na changamoto nyingi katika soka la Zanzibar bado kuna nafasi kufanya soka la visiwa hivyo kutambulika kimataifa.

Bushiri alisema njia pekee ni ile ya uongozi wa ZFA kuandaa mpango maalum wa kuwawezesha vijana kimchezo kwa kuwapa mafunzo sahihi ya soka pamoja kwa kuandaa kituo maalum cha kufanya kazi.

“Njia hii ni wazi kuwa itafanya kijana kuwa na ukakamavu madhubuti pamoja na kuwa na utayari wa kushindana kimchzeo wakati wowote kuliko huu mpango uliopa sasa wa kutafutwa vijana kwa kuunda timu, lakini hakuna maandalizi ya awali kwa upande wao”alisema Bushir.

Alisema kuwa hivi sasa vijana wengi wamekuwa na shauku ya kimchezo, lakini hushindwa kuendelea kutokana na viongozi wa soka visiwani, kukosa njia muafaka ya kuwalea vijana hao kimchezo ili baadae wawe ni tegemeo kubwa katika medani za soka pamoja na kuitangaza Zanzibar.

“Pindi uongozi wa ZFA ukiweka mikakati juu ya kuliinua soka la Zanzibar kwa kuandaa utaratibu mzuri kwa vijana wetu ni dhahiri kuwa itakuwa ni njia pekee ya kuondoka hapa tulipo na kusonga mbele kama walivyo endelea wenzetu katika nchi mbali mbali,” alisema Bushiri.

Hata hivyo, Bushiri amekerwa na mfumo wa Ligi Kuu  Zanzibar akidai unachangia kudumaza soka la visiwa hivyo.

Alisema kuwa umefika wakati kwa ZFA kuandaa ligi moja tu badala ya mfumo uliopo hivi sasa ligi hiyo kuwa na pande mbili yaani kuna timu 14 zinacheza ligi Pemba na nyingine 14 zikicheza Unguja.

Hivyo alisema ili kufanikiwa kwa mipango yote hiyo ni wazi kuwa uongozi wa ZFA unahitajika kukaa chini kwa kushirikiana na wadau wa soka mbalimbali ili kupanga mipango imara itakayoweza kuinua soka la Zanzibar.