Bunduki hizi zaja Yanga

Ahmed Toure.

Muktasari:

  • Zahera atakayekaa benchini Jumapili hii kwa mara ya kwanza kuiongoza Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara, amewasisitizia mabosi wake, kama mashine hizo kutoka DR Congo zitashuka Jangwani, wapinzani wao lazima waombe po!

ACHANA na straika matata wa ASEC Mimosas, Ahmed Toure ambaye jana tuliowadokeza mabosi wa Yanga wameanza kumfukuzia ili atue Jangwani, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi amezitaja mashine nyingine tatu mpya anazozitaka.

Zahera atakayekaa benchini Jumapili hii kwa mara ya kwanza kuiongoza Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara, amewasisitizia mabosi wake, kama mashine hizo kutoka DR Congo zitashuka Jangwani, wapinzani wao lazima waombe po!

Nyota hao ambao Kocha Zahera amewamwagia sifa na kusema wakitua tu, kila kitu ndani ya Yanga kitakuwa shwari ni beki kisiki kutoka AS Vita, Yannick Bangala Litombo na kiungo wa timu hiyo, Fabrice Ngoma.

Kifaa kingine ni straika anayekipiga TP Mazembe, Ben Malongo Ngita na Kocha Zahera alisema anawajua wachezaji hao kwani anawanoa katika timu ya taifa ya DR Congo yeye akiwa kama Kocha Msaidizi na juzi tu alikuwa nao Liberia.

Akizungumza na Mwanaspoti jana Alhamisi mara baada ya mazoezi ya asubuhi ya timu yake, Kocha Zahera alisema kama mabosi wa Yanga wanataka kuwa na timu itakayozitetemesha Simba, Azam na klabuni nyingine zinazofukuzia taji la Ligi Kuu Bara, basi ni lazima wawanyakua wachezaji hao aliowataja.

Alisema kwa kuwa dirisha dogo lipo jirani ni lazima mabosi wake waanze mipango sasa ya kunasa saini ya vijana hao kama pendekezo lake la kuongeza vifaa vipya vya kuchukua nafasi ya watakaotemwa kikosini.

Ingawa Kocha Zahera amekuwa msiri kutaja atakaowatema katika kikosi chake, lakini nusa nusa za Mwaqnaspoti zimebaini kuwa straika Amissi Tambwe na kiungo Thabani Kamusoko siku zao Jangwani zinahesabika kwa sasa.

Kocha Zahera alisema amewafuatilia nyota hao na amebaini kutokana na mahitaji ya kikosi chake kwa sasa endapo atapata wachezaji hao basi hatakuwa na sababu ya kuongeza nyota wengi katika kikosi chake kwa msimu ujao.

“Kwanza wana umri mdogo na kuweza kucheza kwa ufanisi, ningependa kuifanya Yanga iwe moja ya timu tishio ni klabu kubwa hapa Tanzania na Afrika, lakini naona kuna tatizo,” alisema Zahera na kufafanua; “Kumtoa mchezaji kutoka TP Mazembe na AS Vita Club sio kazi rahisi na Yanga imeyumba kiuchumi, lakini kama wanahitaji kikosi bora na cha ushindani ninaamini naweza nikawatafutia wachezaji wengi wastakaoisaidia timu.”

Alisema Malongo, Ngoma na beki Litombo ni wachezaji wazuri ambao wakiungana na vifaa kama Ibrahim Ajibu, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na wengineo kikosini, Yanga itatisha nchini na kimataifa.

APANIA KINOMA

Kocha Zahera amefichua kuwa, kiu yake ndani ya Yanga ni kuona timu inapata matokeo mazuri katika Ligi Kuu Bara ili kurejesha taji walilonyang’anywa na watani zao Simba wanaotarajia kuvaana nao Septemba 30.

“Tuna mechi wikiendi hii na nyinginezo kabla ya kuvaana na Simba, kwa sasa akili ni katika michezo hiyo ya awali ili kukusanya pointi za kutosha, Ligi ya msimu huu ni ngumu na idadi ya timu imeongezeka,” alisema.

Yanga itaikaribisha Stand United Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuvaana na Coastal Union halafu Singida United kisha kucheza na JKT Tanzania na Kocha Zahera alisema amewasisitizia vijana wake washinde mechi zote.

Katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga ilishinda mabao 2-1 huku Zahera akiwa jukwaani kwani hakuwa na vibali vya kumruhusu kuungana na kikosi chake uwanjani.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo Ijumaa kwa mechi mbili ambapo Mwadui ikiwa kwao Shinyanga itaikaribisha Azam FC, huku African Lyon itacheza na Coastal Unioni jijini Dar es Salaam.