Buku moja tu kuiona Mtibwa Sugar na Singida United

Muktasari:

 Mtibwa na Singida wanacheza mechi ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara na mshindi kati ya timu hizo, ataiwakilisha nchi kwenye mashindano Afrika.

Arusha: Kiingilio cha chini katika mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho (FA) utakaopigwa mkoani hapa Juni 2, mwaka huu kwenye  Uwanja wa Sheikh Amri Abeid  ni shilingi elfu moja tu (sh 1,000).
Lengo la kufanya kiingilio hiki ni kwa ajili ya kuwavutia mashabiki wengi zaidi kupata nafasi ya kuona mchezo huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha  (ARFA), Peter Temu amesema, TFF imewataarifu viingilio vya mchezo huo vimegawanywa katika makundi matatu kulingana na uwanja huo ulivyo.
“ Jukwaa kuu kiingilio kitakuwa elfu kumi (sh.10,000), jukwaa B1 na B2  ni shilingi elfu mbili (2,000) na jukwaa C’ ambalo ni mzunguko kiingilio kitakuwa sawa na bure ambacho ni elfu moja (Sh. 1,000),"amesema Temu.
“Kiingilio hiki ni pendekezo la kamati ya ARFA iliyokuta wiki iliyopita na tuliwakilisha TFF hivyo tunashukuru uongozi TFF kwa kukubali mapendekezo yetu”ameongeza Temu.
Amesema, kwa kuwa tiketi za mchezo huo bado hazijawasili ni ngumu kueleza zitaanza kuuzwa lini japo alihaidi zitaanza kuuzwa siku moja hata kabla ya mchezo huo ikiwa ni kutoa fulsa kwa wale wanaoishi mbali hasa wapenzi wa timu ya Singida na Mtibwa.
Temu aliongeza kuwa mpaka maandalizi kuelekea mchezo huo yanaendelea na uwanja unafanyiwa marekebisho kwa kushirikiana na wamiliki, ni pamoja na kupunguza nyasi na kuweka sawa vyumba vya kubadilishia nguo.
Amesema wanatarajia mashabiki mbalimbali kutoka mikoa ya jirani ikiwemo Kilimanajaro, Manyara ,na Arusha na mikoa Mingine watafika kushuhudia na kama ilivyo kwa mikoa ya Singida na Morogoro hamasa kubwa inafanyika.