Brazil mbwembwe kibao

WABRAZILI wana mbwembwe hao, acha tu. Mpango wao ni kwenda Russia kuzima majanga ya fainali zilizopita za Kombe la Dunia zilipofanyika kwenye ardhi ya kwao. Wamepania kunyakua ubingwa huo kwa mara ya sita.

Katika kutimiza mipango yao hiyo, wamefanya mpango wa kuhakikisha kwamba mastaa wao wote wapo fiti kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Dunia zitakazoanza hivi karibuni zikihusisha wababe kibao wakiwamo Ujerumani, Hispania, Ufaransa, Ubelgiji na Argentina. Kwanza walianza kwa kumpigisha tizi la nguvu supastaa wao, Neymar na kisha kwenda kumfanyia vipimo vya afya. Si unakumbuka Neymar ametoka kufanyiwa upasuaji wa mguu? Hivyo Wabrazili wanajaribu kumfanyia vipimo vyote vinavyostahili kuona kama amekuwa kwenye utimamu halisi kwa ajili ya fainali hizo.

Vipimo vya aina hiyo havikuishia kwa Neymar, bali vilifanyika pia kwa mastaa wengine akiwamo beki wa kati wa timu hiyo anayecheza klabu moja pia na Neymar huko Paris Saint-Germain, Thiago Silva.

Vipimo hivyo ilikuwa kuhakikisha kama mastaa hao wapo fiti, hasa kwa Neymar ili wasiharakishe mambo ya kumchezesha mapema na kumweka kwenye wakati mgumu zaidi kwa kumwongezea matatizo.

Ule wasiwasi juu ya Neymar bado upo kwa sababu yale majeraha yaliyotishia ushiriki wake kule Russia, hivyo ndiyo maana kumekuwa na jitihada hizo za makusudi kumpata staa huyo aliyenaswa kwa Pauni 198 milioni.

Mpango ni kutambua kama mshambuliaji huyo yupo fiti kabla ya kutupa karata yao ya kwanza kwenye fainali hizo kwa kukipiga na Uswisi, Juni 17.

Neymar, 26, aliwekewa oksijeni na kubandikwa nyaya kibao mwilini akiwekwa kwenye mashine ya kukimbilia, ili kutambua utimamu wa mwili wake. Kwenye vipimo kila kitu kilionekana kuwa sawa, hivyo mambo ni moto.

Wakati Neymar akifanyiwa vipimo hivyo, staa mwingine wa kikosi hicho, Philippe Coutinho, aliwasili kwenye kambi ya timu ya taifa kistaa kwa helikopta ya kukodi, kisha akapandishwa kwenye gari maalumu, iliyopigwa chata za Brazil kwenda kuungana na wenzake.

Staa huyo wa zamani wa Liverpool, ameonekana kuwa fiti katika siku za karibuni baada ya uhamisho wake wa kutua Barcelona kwenye dirisha la usajili wa Januari.

Brazili itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Croatia Juni 3 na inaamini Neymar na mastaa wengine kama Coutinho watakuwa fiti kucheza mechi hiyo, wiki mbili kabla ya kumenyana na Uswisi katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia.

Neymar alisema: “Hakuna mtu mwenye wasiwasi zaidi kuliko ilivyo kwangu. Najua watu wana wasiwasi, lakini hakuna mwenye hofu kuhusu kurejea uwanjani kuliko mimi mwenyewe. Kimekuwa kipindi kigumu sana kwangu, pengine hiki ni kitu kigumu kuwahi kunitokea kwa sababu imekuwa karibu na fainali za Kombe la Dunia.

“Namshukuru Mungu kwa nafasi hii ya ziada, nafasi ya kwenda kusaka ubingwa wa dunia na nchi tangu, kitu ambacho kimekuwa kwenye ndoto zangu tangu utotoni. Ni lengo langu, natumaini huu ni ubingwa wangu.”

Neymar alikuwa na msimu mzuri huko Ufaransa kabla ya mambo kuja kuharibika kutokana na kuumia mguu. Lakini, jambo hilo halikumzuia kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwenye Ligue 1 licha ya kukosa mechi kadhaa za mwishoni mwa msimu, akifunga mabao 19 na kuasisti 15 kwenye ligi hiyo.