Bosi wa Villareal amwaga vifaa vya michezo kwa Polisi

Arusha. Timu ya soka Mkoa wa Polisi imepokea jezi 25 kutoka kwa mmoja wa wakurugenzi wa timu ya Villareal inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania, Ammar Hiyani Roig ambaye ameeleza kuendelea kusapoti Jeshi la Polisi upande wa michezo.
Roig alisema kwamba alishuhudia timu ya Polisi Morani mwaka jana ikiwa kwenye ligi ya Mkoa wa Arusha jambo ambalo lilimfurahisha kuona askari wanashiriki michezo pamoja na raia kwenye michezo kitendo kilicho mfurahisha.  
 
“Ili soka lenu likuwe lazima kuwe na ushirikiano mzuri na timu  mbalimbali kutoka mataifa ya nje na hii itawafanya kujifunza mambo mengi kutoka kwao na ninaami kwa ushirikiano wa nchi hii ilivyo mtafanikiwa haraka.”
“Tanzania ni moja ya nchi yenye amani ndio maana napenda kuja kutalii na familia yangu kila ninapopata nafasi baada ya mapumziko ya soka ya Ligi Kuu nchini Hispania hivyo ni wakati wa Polisi nao kuwa na timu Ligi kuu Tanzania,” alisema Roig.
Aliongeza kuwa Tanzania ni moja ya nchi yenye vipaji vingi vya soka hivyo  vinatakiwa watu wa kuviendeleza kama  mataifa mengine yanavyofanya, huku akieleza kutomjua Mbwana Samata licha ya kulisikia jina hilo likitajwa hapa nchini.
Wengine aliotanguzana nao ni pamoja na Abdulhakim Mullam Dadkareem Mulla pamoja na Ilyas Mulla ambao ni familia moja waliochangia kumshawishi bosi huyo wa Villareal kumwaga vifaa vya michezo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhan Ng’anzi alisema wataendelea kukiimalisha kikosi cha timu hiyo ili wafanye vyema msimu ujao wa Ligi ya Mkoa wa Arusha ilikupata nafasi ya kuelekea SDL na FDL na hatimaye Ligi Kuu.
Ng’anzi aliongeza kuwa watazidi kuwa karibu na bosi huyo ili kuona anakuwa balozi wa timu hiyo katika kufanikisha michezo katika timu za Jeshi la Polisi.