Bosi ZFA achimba mkwara

Thursday October 12 2017

 

By HAJI MTUMWA, UNGUJA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Mohamed Hilal ‘Tedy’ ameapa kuwashughulikia waamuzi watakaoboronga mechi za Ligi Kuu Zanzibar zinazoendelea visiwani hapa.

Tedy alisema pamoja na kwamba ligi hiyo ipo katika hatua za awali, tayari kuna baadhi ya waamuzi wameanza kulalamikiwa kwa uchezeshaji usiofuata sheria na yeye kaamua kuwaonya mapema ili wasije wakalaumiana mbele ya safari.

“Tukibaini tuhuma dhidi ya waamuzi wetu zina ukweli, hatutasita kumchukulia hatua mhusika, tutafanya hivyo ili kulinda ligi yetu kuingia katika migogoro ambayo inaepukika,” alisema Tedy.

Pia alisema ZFA haitomvumilia kocha yeyote ambaye anafundisha soka bila ya kuwa na vibali sahihi za ufundishaji.

Alisema kwa mujibu wa sheria za soka visiwani Zanzibar, kocha lazima awe na Leseni Daraja B ndio awe halali kunoa timu ya Ligi Kuu.