Bosi Hans Poppe amlipua Kapombe Simba

Tuesday November 14 2017

 

By OLIPA ASSA

KAULI ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ni kama imemuweka njia panda beki, Shomary Kapombe. Poppe kasema Kapombe amepona ila hataki kutumika.

“Kapombe amepona ila uoga wake mwenyewe, achugue kama anataka kubaki ama akae pembeni hadi atakapokuwa tayari kutumika, la sivyo maamuzi yake mikononi mwake ,” alisema Hans Poppe alipozungumza na kituo kimoja cha redio.

Lakini mtu wa ndani wa Simba, alionesha kushangazwa na kauli ya Poppe akisema bosi huyo anajua wazi walimsajili Kapombe kutoka Azam akiwa majeruhi, hivyo kutamka kauli hiyo ni kumuonea.

“Ninachojua mimi Kapombe bado anaumwa na lengo la kumsajili ilikuwa ni kwa ajili ya michuano ya kimataifa, sasa inapotokea anaambiwa hivyo ni kama kumuongezea machungu na kumuondoa kabisa kwenye mstari,” alisema mtu huyo wa ndani.

“Nadhani hadi kufikia Januari anaweza kuwa na mwelekeo mzuri, ila bado anasumbuliwa labda daktari aseme vipimo vyake vinasemaje.”

Kapombe mwenyewe alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo, hakutoa ushirikiano. Alipotafutwa Daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe, ili kuelezea hali ya bekji huyo, hakupokea simu yake.