Bondia Mtanzania apanda ulingoni England

Muktasari:

 Feriche ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Super Light), amesema kuwa hii ni fursa kwake kuonyesha kipaji chake nje ya nchi

Dar es Salaam. Baada ya bondia wa Tanzania, Hassan Mwakinyo kumchapa kwa Technical Knock Out (TKO), Sam Eggington wa England Septemba 8, sasa bondia nyota mwanamke wa Tanzania, Feriche Mashauri jioni ya leo Jumamosi anapanda ulingoni kukipiga na Nina Bradley mjini Leicester.

Feriche anawania Ubingwa wa Jumuiya wa Madola wa uzito wa Super-lightweight katika pambano la raundi 10, kwenye ukumbi wa King Power Stadium.

Feriche ambaye hajapoteza pambano hata moja kati ya sita aliyocheza, ametamba kumchapa mpinzani wake ambaye pia ameshinda michezo yote mitano aliyocheza.

“Nimejiandaa vizuri na natarajia kushinda, nimepata muda mwingi wa maandalizi hivyo hakuna kitakacho nishinda. Awali nilikataa mapambano mbalimbali nyumbani lengo lilikuwa ni kufanya vizuri hapa London na nitampiga,” alisema Feriche na kusisitiza anaujua ugumu wa pambano hilo.

Amesema, amehamasika na ushindi wa Mwakinyo na anaamini atafanya kama alivyofanya Mtanzania mwenzake.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kupigana nje ya Tanzania, lazima nitumie fursa hii ipasavyo na kuipromoti nchi Yangu,” alisisitiza Feriche.