Bocco akubali yaishe kwa Okwi

Muktasari:

Okwi kwa sasa anaoongoza kwa ufungaji mabao akiwa amezifumania nyavu mara 19

Dar es Salaam. Simba sasa ni mwendo wa kukaba mpaka kivuli na ipo hivi, John Bocco hataki uchoyo kabisa, alipoona Emmanuel Okwi anaongoza kwa mabao ya kufunga, ameamua kumtengenezea njia ya kuhakikisha anatupia kila mechi.

Kati ya mambo anayoyafanya Bocco ni kumwachia Okwi apige faulo na penalti, wakati mwingine kumtengezea nafasi za kufunga anapomwona amekaa vizuri ndani ya 18, lengo anataka awe na idadi kubwa ya mabao.

Bocco amesema, haoni sababu ya kufanya uchoyo pindi anapomwona Okwi yupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga kwa sababu kila mtu yupo kwa ajili ya manufaa ya Simba na si ya mtu binafsi.

"Okwi ndiye anayeongoza kwa mabao, lazima kama tuna namna yoyote ya kumwezesha tumpe ushirikiano ili tuweze kuandika rekodi ya aina yake msimu huu.

"Sina maana kwamba ninapopata nafasi ya kufunga nitajibweteka, napambana lakini lengo ni kutwaa ubingwa ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wetu," anasema Bocco ambaye amefunga mabao 14.

Bocco anasema kitu pekee anachokiona kitawawezesha kufikia malengo ni ushirikiano wa hali na mali na kujua wapo kwa ajili ya timu: "Sichezi ili mimi nionekane bora kuliko mwingine isipokuwa natimiza kile kilichonileta Simba na ndivyo ilivyo kila mchezaji anatakiwa kuwa hivyo,"anaeleza.

WENGINE WAMTAJA

Wakati huo huo; Kocha msaidizi wa Majimaji ya Songea, Habibu Kondo amemtaja Okwi wa Simba kuwa mchezaji hatari wa kuzifuma nyavu hasa watakapokutana mechi ya mzunguko wa pili baada ya raundi ya kwanza kufungwa mabao 4-0.

"Okwi ni mchezaji anayefunga kwa mahesabu na kuwahadaa mabeki, lazima aangaliwe kwa jicho la tofauti siku tutakapocheza nao mechi," anasema Kondo.

Kocha wa Ndanda FC, Malale Hamsini anasema kikosi kizima cha Simba kipo moto, lakini Okwi amemwona ana mipango ya kuzisakama nyavu za wapinzani, hivyo ni mchezaji  atakayetazamwa kwa jicho la ndani katika mechi yao.

"Ligi ni ngumu ni afadhari ucheze na Simba na Yanga kwa sasa, kuliko tukakutana wenyewe, lakini kuhusu Okwi ni mchezaji mzoefu ambaye anajua nini anataka katika ligi," alisema Malale.