Simba yaifanya kitu mbaya Prisons

Muktasari:

Kutokana na matokeo hayo, Simba imeendelea kujichimbia kileleni baada ya kufikisha pointi 22,ikiwa pointi tano mbele dhidi ya wapinzani wao wakubwa Yanga ambao kesho wataikabili Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Bao la mshambuliaji John Bocoo limetosha kuifanya Simba kuondoka na pointi sita mkoani Mbeya baada ya kuifunga Prisons kwa bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Kutokana na matokeo hayo, Simba imeendelea kujichimbia kileleni baada ya kufikisha pointi 22,ikiwa pointi tano mbele dhidi ya wapinzani wao wakubwa Yanga ambao kesho wataikabili Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Bocco'Adebayor'alipeleka kilio Prisons baada ya kufunga bao kwa shuti kali dakika ya 84 na kumshinda kipa Aron Kalambo aliyeruka kuokoa mpira huo bila mafanikio.
Ushindi huo unaifanya Simba kuweka rekodi bora msimu huu  jijini Mbeya baada ya kuondoka na pointi zote sita dhidi ya timu mbili za mkoa huo kwani wiki mbili zilizopita iliichapa Mbeya City bao 1-0.
Katika michezo mingine kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi,Ruvu Shooting walipata ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kuifunga Ndanda bao 1-0.Bao la washindi lilifungwa na Abdulrahaman Musa.
Uwanja wa Majimaji Songea,wenyeji Majimaji waliifunga Mbao mabao 2-1. Mabao ya Majimaji yalifungwa na Jafar Mohammed nna Marcel Boniventure kwa penalti.
Kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga,Stand United ilitoka suluhu na Mwadui.
Ligi Kuu itaendelea kesho Jumapili kwa Yanga kuikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Kagera Sugar itakuwa ugenini kuumana na ndugu zao Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Turiani Morogoro, Azam itakuwa mgeni wa  Njombe Mji kwenye Uwanja wa Sabasaba Njombe.