Bocco: Nawasubiri, nitawalaza mapema

Muktasari:

Taifa Stars ambayo jana usiku ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria, pia ataukosa mchezo dhidi ya DR Congo, lakini yuko mafichoni akisaka tiba ya kuwaliza Jangwani.

MABEKI wanamjua sana huyo jamaa kwani, ana nguvu, anamiliki mpira na anajua kupasia nyavuni. Iko hivi, straika na nahodha wa Simba, John Bocco ameachwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kutokana na kuwa majeruhi.

Taifa Stars ambayo jana usiku ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria, pia ataukosa mchezo dhidi ya DR Congo, lakini yuko mafichoni akisaka tiba ya kuwaliza Jangwani.

Bocco, ambaye ametupia mabao 10 mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara, alipata maumivu ya paja kwenye mchezo dhidi ya Al Masry nchini Misri, anataka kumaliza hasira zake kwa Yanga.

“Nimeshindwa kujiunga na Taifa Stars ili nipate muda wa kupumzika na kujifua mwenyewe, lakini nataka nimalize hasira zangu kwa Yanga.

“Hadi ligi ikianza na mchezo wetu na Yanga utakuwa karibuni sana, nitakuwa fiti na nataka kuisaidia Simba kufanya vizuri na kubeba taji msimu huu,” alisema Bocco.

Kwa sasa straika huyo wa zamani wa Azam FC, anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wapachika mabao nyuma ya Emmanuel Okwi wemye mabao 16 na Obrey Chirwa wa Yanga (mabao 12).

Afunika mabao

Hata hivyo, mabao yake hayo Bocco, amewafunika kabisa mastraika wanne wa Azam ambao waliletwa kikosini hapo kuziba pengo lake baada ya kutimikia zake Simba.

Mastraika wa Azam FC ukiwachanganya ndio wanafikia idadi ya mabao ya Bocco, ambapo Yahya Zayd ana mabao manne, Mbaraka Yusuph (3), Shaban Idd (1) na Mghana Bernard Arthur (2). Pamoja na Bocco, kuwaburuza kwa idadi hiyo, lakini bado hawajaweza kuvunja rekodi yake alioiacha ya mabao 11 kabla ya kutimkia Simba.

Kwa upande wake, Mbaraka alisema hilo la kufunikwa na Bocco inawaumiza, lakini jambo la msingi kwao ni pointi na sio mabao tu.

“ Azam ipo nafasi za juu na ndilo jambo tulilolizingatia, lakini tunahitaji kujipanga ili tuwe na mabao mengi, inapotokea tukagongana na timu nyingine basi tuwe na nafasi nzuri,” alisema.