Bizimungu aona kitu kwa Ditram

KOCHA wa Mwadui FC, Ally Bizimungu amekiangalia kipaji cha straika wa Azam FC, Ditram Nchimbi na kukiri kama ataongeza juhudi kidogo tu basi atyaingia anga za Mbwana Samatta ama Simon Msuva kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Bizimungu alikuwa akimwinda nyota huyo aliyekuwa Njombe Mji ili atue Mwadui, lakini Azam wakampiga bao.

“Nimeanza kumfuatilia muda mrefu Ditram, akiamua kuelekeza nguvu zaidi katika soka anaweza kuuzwa kwa bei ya juu nje ya nchi, kwa sababu yupo vizuri mno, ndio maana nilikuwa namsaka ili nimsajili,” alisema Bizimungu anatokea Rwanda.

“Na chipukizi mwingine niliyekuwa namtani niwe naye ni Shaaban Idd aliyepata dili nje ya nchi, ila kwa Ditram naamini akiendelea na kasi ile basi, ataonekana na timu za Ulaya,” alisema.

Kuhusu ongezeko la timu za Ligi Kuu kutoka 16 hadi 20 alisema itasaidia kuwapa nafasi vijana wake kucheza kwa muda mrefu.

“Uzuri wa ongezeko wa mechi ni kuwa na vijana wataendelea kupata uzoefu wakati ligi inaendelea, ni kweli wanaweza wakaanza ovyo lakini kadri siku zitakavyokuwa zinaenda watakuwa wanaimalika,” alisema Bizimungu.