Kocha Bilo: Sirudi tena Stand United

Muktasari:

Bilo anamaliza adhabu yake kesho Jumatano, tangu aliposimamishwa na uongozi wa Klabu hiyo kwa siku 30, kwa madai ya utovu wa nidhamu Oktoba 22 siku ambayo Stand ilikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga.

Mwanza. Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’ amesema hana mpango wa kuendelea na timu hiyo baada ya kumaliza adhabu yake.
Bilo anamaliza adhabu yake kesho Jumatano, tangu aliposimamishwa na uongozi wa Klabu hiyo kwa siku 30, kwa madai ya utovu wa nidhamu Oktoba 22 siku ambayo Stand ilikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga.
Akizungumza baada ya mazoezi yake na timu ya Toto Africans kwenye Uwanja wa Mirongo jijini hapa, kocha huyo alisema hana mpango wa kurudi kwa Wapiga debe hao.
Alisema yeye na familia yake wamekaa na kutafakari na kuamua kuwa asirudi kwani hiyo ni fedhea na kwamba anataka aondoe dharau ambayo imekuwa sugu.
“Hii siyo mara ya kwanza Stand kunisimamisha, hata msimu uliopita walinifanyia hivi nikakaa nje kwa miezi miwili, kwahiyo msimamo wangu sirudi kabisa”alisema Bilo.
Aliongeza kuwa yeye ni kocha mwenye taaluma,hivyo atapumzika kwanza, huku akiwa anaendelea na mazoezi na kwamba hata Toto Africans wakimhitaji yuko tayari kwa makubaliano.
“Nitakuwa nafanya mazoezi yangu hapa Mirongo na Toto asubuhi, kisha jioni nakuwa na timu ya Maveterani, lakini wakati huo nitakuwa nasikilizia msimamo wao pia,”alisema Kocha huyo aliyewahi kukipiga Toto Africans.
Mwenyekiti wa Stand United, Dk Heryson Maheja alisema wao wanasubiri siku ifike ili alete utetezi wake wa kimaandishi kwenye kamati kisha uamuzi yatolewe.
“Alitakiwa alete utetezi wake kwa maandishi kujibu tuhuma zake, kisha kikao cha kamati kiamue, kama hatokuja ni uamuzi wake na kamati itakaa na kutumia busara kufanya uamuzi,” alisema Maheja.