Bifu la Rojo, Sanchez kaa mbali nao

MANCHESTER, ENGLAND
BEKI wa Manchester United, Marcos Rojo amesema si kitu alichokipokea vizuri kuhusu usajili wa Alexis Sanchez.
Si unajua Rojo na Sanchez picha huwa haziendi kabisa. Mara zote walizokutana wamekuwa wakipigana sana rafu, iwe kwenye timu zao za taifa au kwenye klabu zao Arsenal na Man United.
Lakini sasa bifu lao linapaswa kumalizika kutokana na kuwa wachezaji wa timu moja na Kocha Jose Murinho amemwambia asithubutu kumchezeana rafu mazoezini.
Kwa sasa Rojo na Sanchez watazungumza na kucheka, lakini hicho si kitu kilichowahi kutokea huko nyuma.
Rojo, ambaye amesaini kuichezea Man United hadi mwaka 2021, alisema: “Alexis ni mchezaji mahiri, lakini hatukuwahi kuwa marafiki si ndani wala nje ya uwanja. Tunapokutana kwenye mechi ni mwendo wa kuchezeana rafu tu. Zaidi ya hilo limekuwa nikimtolea lugha mbaya na yeye pia anajibu mapigo.
“Hivyo nilipogundua  anajiunga na United, nilisema: ‘Oh, dah, huyu mtu anakuja hapa.’ Tulikuwa Dubai kipindi usajili wa Alexis ukikamilishwa. Nilikuwa nimeketi kimya kwenye kiti ndipo Kocha Jose Mourinho alipokuja na kunigusa kwenye beki, akiniambia: ‘Tunamsajili Alexis. Sitaki umchezee rafu mazoezini.’ Kisha akaangua kicheko.”
Wakati huo huo, Sanchez mwenyewe amefunguka na kudai mambo aliyoyatarajia wakati anatua Man United hayakwenda kama alivyopanga. Staa huyo amefunga bao moja tu katika mechi 10 alizocheza kwenye timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.