Biashara United yasajili wanne Azam

Muktasari:

  • Biashara ya Mara, ilimaliza mechi zake tisa ikiwa nafasi ya tatu na pointi 17, inatanguliwa na Dodoma FC  wenye pointi 18 na Alliance FC wanaoongoza Kundi C kwa pointi 19.

Biashara FC imedhamiria kupanda Ligi Kuu msimu ujao baada ya kuamua kuchukua wachezaji wanne kutoka  Azam B, ili kukiongezea nguvu kikosi chao.

Biashara ya mkoani Mara, ilimaliza mechi zake tisa ikiwa nafasi ya tatu na pointi 17, inatanguliwa na Dodoma FC  wenye pointi 18 na Alliance FC wanaoongoza Kundi C kwa pointi 19.

Kocha msaidizi wa Biashara, Aman Josiah alisema, katika kipindi hiki cha dirisha dogo wanatarajia kuongeza wachezaji wanne kwenye nafasi tofauti ili kuwa na kikosi kipana na kufikia malengo yao.

Josiah alisema wachezaji hao ni kutoka Azam kikosi B, ambao watawaleta kwa mkopo na kwamba

wameridhishwa na uwezo wao na uongozi umeridhia kuwaruhusu.

"Muda wowote kuanzia sasa (jana) watawasili kambini kuungana na wenzao, nia na dhamira yetu ni kucheza ligi kuu msimu ujao, hatupambani na timu moja sisi tutaenda kimya kimya," alisema Josiah.

Kocha huyo aliwataja wachezaji hao ni pamoja na kiungo, Stanslaus Lujage, mshambuliaji Rajabu Odasi na mabeki Ally Khatib na Abas Kapombe aliyeitwa timu ya Taifa ya vijana (U-23).

"Sisi hatutarajii kuacha mchezaji yeyote labda yule atakayeonekana kutokuwa na nidhamu, lakini si kwamba atakayeshuka kiwango," alisema kocha huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Azam FC, Jafari Idd Maganga alisema hajapata taarifa ya nyota hao

kutimkia Biashara na aliahidi kufuatilia ina kutoa taarifa.

"Binafsi sijapata taarifa hizo na huenda ni kutokana na majukumu niliyonayo, lakini nitafuatilia kama ipo

nitapata ukweli na nitatoa taarifa," alisema Maganga.