Beckham, Sakho walivyopishana Serengeti

Muktasari:

Wengi haiwaingii akilini kabisa. Wanauangalia ule ustaa wa Beckham, nyota wa zamani wa Manchester United na England kwa jumla ambaye kimsingi ndiye staa wa soka aliye tajiri zaidi duniani.

KUNA watu wanajiuliza, ilikuwaje David Beckham, pamoja na umaarufu wake wote alifika Tanzania na kisha kuondoka kimyakimya alipofanya ziara ya kitalii hivi karibuni?

Wengi haiwaingii akilini kabisa. Wanauangalia ule ustaa wa Beckham, nyota wa zamani wa Manchester United na England kwa jumla ambaye kimsingi ndiye staa wa soka aliye tajiri zaidi duniani.

Walitarajia ujio wake ungetawaliwa na kamera za vyombo vya habari mwanzo mwisho.

Haikuwa hivyo na ilikuwa kimya kimya kwa sababu ndivyo alivyotaka mwenyewe.

Hata hivyo, Mwanaspoti limefanikiwa kunusa kwa ukaribu ziara ya staa huyo aliyefika kwa mapumziko mafupi kwenye mbuga ya wanyama ya Serengeti akiwa na familia yake; mkewe Victoria pamoja na wanawe wote wanne, Brooklyn, Romeo, Cruz na Harper Seven.

Ni kama ilivyo kwa staa mwingine, Mamadou Sakho, Mfaransa aliyewahi kukipiga Liverpool, naye alifika na familia yake, mkewe Majda na watoto wao; Sienna na Aida.

Maisha ya Beckham Serengeti

Beckham alikuwa na ziara ya mapumziko ya siku saba nchini kuanzia Mei 27 hadi Juni 3 na siku zote hizo alizitumia mbungani Serengeti, akijionea wanyama mbalimbali.

Ujio wake haukutangazwa kabisa kwa mujibu wa utaratibu ulivyopanga, hata hivyo, uwepo wake baadaye ulianza kuvuja katika mitandao ya kijamii.

Alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaan na kisha kwenda Arusha kwa ndege ndogo ya kukodi.

Wahudumu wamshangaa

Mmoja wa wahudumu katika hoteli ya kitalii ya Serengeti iliyopo mbugani humo ambapo Beckham alifikia, alisema taarifa zilipowafikia juu ya ujio wa nyota huyo hawakuamini.

“Wengi tulikuwa na shauku ya kutaka kumwona, lakini tulivyoona barua yake ilionyesha ni mgeni wa daraja la juu kabisa (VVIP), hivyo tukajua haitakuwa rahisi kwani atakuwa na ulinzi wake binafsi,” anasema mhudumu ambaye alikataa kutajwa jina.

“Hapa alifika jioni, hivyo haikuwa rahisi kuanza mazoea, ni tofauti na wanapokuja Waafrika wenzetu wao huwa ni rahisi kumjua mtu tabia yake. Hawa wenzetu (Wazungu) wakifika hapa wanakuwa bize na mambo yao.”

Maisha yake mbugani

Mhudumu huyo anasema Beckham alikuwa akiamka mapema zaidi kuliko hata mkewe na kuanza kuzunguka zunguka huku na kule akiangalia mazingira ya hoteli kabla ya kupata kifungua kinywa.

“Hapa kuna vyakula vya aina nyingi vinavyowekwa mezani, mteja anajichagulia mwenyewe anachokipenda. Kwetu ilikuwa ngumu kujua alikuwa anakula nini kwani si maadili ya Mtanzania kumwangalia mtu anapokula,” anasema.

Hata hivyo, anasema kabla ya kula, Beckham alipenda kuanza kunywa kahawa halafu ndipo huifuata familia yake chumbani kwa ajili ya kifungua kinywa cha pamoja, baada ya hapo dereva huwafuata na kwenda mbugani kuangalia wanyama.

Jamaa hapendi masihara

“Alikuwa mwongeaji, alipiga stori lakini hakutaka masihara. Mambo ya kupiga naye picha hakuyataka kabisa. Alikuwa tofauti na wageni wengine ambao wao huwa tayari kupiga picha na yeyote,” anasema mhudumu huyo.

“Lakini alionyesha kuyafurahia sana maisha hapa. Hata watoto wake kwani mara nyingi walikuwa wakizunguka zunguka kuangalia mazingira ya Kitanzania na kuyafurahia mno.”

Sakho apishana na Beckham

Siku mbili tu baada ya Beckham na familia yake kuondoka, akawasili Sakho, staa mwingine wa soka naye akiwa na familia yake.

Hata hiyo, ujio wa Sakho ulijulikana haraka tofauti na wa Beckham, ingawa kwa Sakho haikufahamika anakwenda wapi kwani kuna waliosema anakwenda kupanda Mlima Kilimanjaro.

Mmoja wa waongoza watalii katika mbuga ya Serengeti, alisema hawakutegemea kumwona mchezaji huyo maana walichoambiwa ni kuwa wanatakiwa kumfuata mgeni hotelini na kumtembeza, hawakuambiwa ni nani.

“Alipofika hapa kwanza tukapatwa na mshangao, tukaacha kazi zetu tukakimbilia kuomba tupate picha angalau za ukumbusho, yeye alitukubalia tukafanya kama tulivyotaka, kisha akaondoka kwenda Camp ya Gurumet Expedition inayoitwa Lemala ambako hata Beckham nasikia alienda huko,” anasema mwongoza watalii huyo ambaye naye aliomba kutotajwa jina.

Wanyama wampagawisha Sakho

Mwongozaji huyo anasema kilichomfurahisha Sakho ni kuwaona wanyama laivu tofauti na alivyozoea kuwatazama kupitia runinga au kwenye majarida.

“Kumbe sisi Watanzania tuna bahati sana kuwa na vitu vya asili. Hawa wenzetu inawezekana hata mgomba wakaushangaa,” anasema.

Sakho ana stori kwenda mbele

Mwongoza watalii huyo anasema Sakho muda wote alikuwa mtu wa stori za hapa na pale, hakusita hata kuwaelezea msimamo wake wa soka baada ya kutoka Liverpool na kutua Crystal Palace kwa mkopo.

“Alisema amefanya hivyo kuhakikisha anapata namba ili aweze kurudi kwenye makali yake.

“Kumbe hawa watu ni wacheshi sana, anazungumza kama mtu wa kawaida tu,” alisema.

Somo kwa wanasoka wa Bongo

Mwongoza watalii huyo anasema amejifunza kitu cha tofauti sana kwa wachezaji hao akiwalinganisha na wanasoka wa Tanzania, akisema hawa wao wanapaswa kujifunza tabia hiyo na kutembelea vivutio vya kitalii wanapukuwa mapumziko kama kipindi hiki ambapo Ligi Kuu Bara imemalizika.

“Unajua tuna sera ya utalii wa ndani, wachezaji wetu nao wanaweza kufanya hivi tena kwa gharama ndogo kabisa.

“Hata hivyo, ninashangaa hatuwaoni kabisa, nadhani kuna namna wanapaswa kushauriwa. Inafaa kuja huku kupumzisha akili zao baada ya kazi ngumu ya uwanjani msimu mzima.”