Becham aibuka na Inter Miami

Muktasari:

  • Baada ya kukamilisha taratibu mbali mbali ikiwemo kusajili nembo na kutambulisha rangi za jezi zitakazotumiwa na klabu hiyo, Beckham ameipa timu hiyo jina la, Club Internacional de Futbol Miami au kwa kifupi Inter Miami CF.

Baada ya nyota wa zamani wa Manchester United na England, David Beckham, kufanikiwa kuanzisha klabu ya soka nchini Marekani mamlaka zimesema itaruhusiwa kucheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (MLS) katika msimu wa mwaka 2020.

Baada ya kukamilisha taratibu mbali mbali ikiwemo kusajili nembo na kutambulisha rangi za jezi zitakazotumiwa na klabu hiyo, Beckham ameipa timu hiyo jina la, Club Internacional de Futbol Miami au kwa kifupi Inter Miami CF.

“Tunafurahi, hatimaye tumekamilisha usajili wa klabu yetu, ambayo ilipata usajili rasmi Januari mwaka huu na yalibakia mambo madogo  kukamilisha na sasa kila kitu kipo tayari kwa kifupi itaitwa Inter Miami CF, tunaomba sapoti kutoka kwa mashabiki,” alisema Beckham.

Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid, Paris St-Germain na AC Milan na nahodha wa zamani wa England, ndiye mmiliki na Rais wa klabu hiyo ambaye amechagua nembo yenye rangi ya pinki, nyeusi na nyeupe ikiwa na picha ya ndege wawili, jua na miale saba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Jorge Mas, aliwasihi mashabiki wote wa soka wa mji wa Miami kuiunga mkono kwa dhati timu hiyo ya nyumbani akisema wanatarajia itakuwa moja ya timu kubwa za soka nchini Marekani.

Alisema wanajivunia mapenzi ya wana Miami wote na kwamba wameridhishwa na mapokezi ya timu hiyo wanaamini wataiunga mkono na kuifanya kuwa moja ya timu kubwa za soka duniani miaka michache ijayo.