Bato la Yanga, Rayon ni noma

Muktasari:

Yanga imejikuta ikiendelea kusota kwenye kusaka matokeo ya ushindi kuanzia Ligi Kuu mpaka kwenye mashindano ya kimataifa.

HALI Yanga si shwari. Dakika 90 za mechi yao ya Jumatano usiku dhidi ya Rayon Sports zilithibitisha kuwa kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria nchini, kinahitaji mabadiliko makubwa.

Yanga imejikuta ikiendelea kusota kwenye kusaka matokeo ya ushindi kuanzia Ligi Kuu mpaka kwenye mashindano ya kimataifa. Suluhu dhidi ya Rayon juzi Jumatano ilikuwa kama msumari wa moto kwenye kidonda kibichi.

Mchezo wa kwanza wa mechi hizo za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ilifungwa mabao 4-0 na USM Alger. Haikuwa na jipya sana. Ilizidiwa mchezo wote. Ilishambuliwa kama simba aliyejichanganya kwenye kundi la nyati.

Mechi ya Jumatano, imeifanya Yanga kufikisha mechi ya nane bila kupata ushindi tangu ilipoondokewa na aliyekuwa kocha wake mkuu, George Lwandamina. Inahuzunisha sana. Timu ya Wananchi imekwama na haina dira.

Ujio wa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera bado haujawa na tija kubwa kwani, timu hiyo imeendelea kuwakosa wachezaji muhimu kama Donald Ngoma na Papy Tshishimbi huku Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko bado hawajawa fiti.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo yaliyojionyesha kwenye mechi ya juzi Jumatano.

KASI YA WACHEZAJI

Wachezaji wa Yanga katika michezo ya awali walikuwa wanaonekana kama wazito, lakini tangu Zahera amewasili klabuni hapo, kasi ya nyota hao imeongezeka zaidi.

Katika mechi dhidi ya watani wao Simba, licha ya kocha huyo kukaa jukwani lakini katika kambi ya Morogoro alikuwa akisimamia mazoezi huku akiwataka wachezaji wake wacheze kwa kasi kubwa na kujiamini.

Kuanzia mchezo huo mpaka ule wa USM Alger wachezaji wa Yanga walikomaa, lakini bado miili yao ilikuwa haijanyumbulika. Hawaonyeshi ungangari.

Kwenye mechi dhidi ya Rayon kasi iliongezeka zaidi. Walikuwa wakipitisha mipira kwa mawinga wao Juma Mahadhi na Geofrey Mwashiuya, lakini umaliziaji ndio ulionekana kuwa tatizo kubwa. Chirwa hakuwa makini katika umaliziaji kwani, mara kwa mara alikuwa anafika golini, lakini umakini wake ulikuwa mdogo.

SAFU YA ULINZI SAFI

Kurejea kwa Kelvin Yondani kumeongeza umakini katika safu ya ulinzi. Mchezo wa kwanza ambao safu ya ulinzi alicheza Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kulionekana kabisa hakuna maelewano mazuri.

Lakini kwenye mchezo na Rayon, Yanga ilionekana kabisa imekomaa na kucheza kwa maelewano ya hali ya juu, huku ikiondoa mashambulizi ambayo yalikuwa yanafika mara kwa mara langoni mwao.

Yondani ambaye alikuwa nahodha katika mchezo huo, alikuwa akiipanga vizuri safu yake ya ulinzi na kuhakikisha haitetereshwi.

Rayon nayo licha ya kwamba ilikuwa ikitengeneza nafasi, lakini katika upande wa umaliziaji ilionekana nayo haikuwa makini baada ya kukosa mtu sahihi katika umaliziaji.

CHIRWA, MHILU BADO

Majeruhi yamekuwa yakiitibulia sana Yanga msimu huu. Katika safu ya ushambuliaji imekuwa ikiwachezesha muda mwingine watu wasiocheza nafasi hizo.

Kukosekana kwa, Ngoma na Tambwe ambao wamesumbuliwa na majeraha kwa muda mrefu, kumeifanya timu hiyo kuhangaika katika kupata mabao msimu huu.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya USM Alger, katika nafasi ya ushambuliaji Yanga ilimchezesha Geofrey Mwashiuya na Yusuph Mhilu, ambao wamezoeleka kucheza nafasi ya winga. Licha ya kucheza kwa kuelewana, walionekana kutotumia vizuri nafasi ambazo walizotengenezewa.

Mechi dhidi ya Rayon Sports Yanga, ilimchezesha Mhilu na Chirwa, lakini hawakuendana kwani mara kwa mara walikuwa hawaelewani katika kujipanga katika nafasi.

Mhilu alikuwa anashuka chini sana kuchukua mipira, lakini hata hivyo, bado pengo la Ngoma na Tambwe lilikuwa likionekana dhahiri.

KAMUSOKO SAFI

Kiungo Mzimbabwe, Thabaan Kamusoko ambaye alikosekana muda mrefu uwanjani baada ya kupata maumivu ya goti, amerejea na huenda akawa tishio tena.

Katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Kamusoko alionekana kurudi upya baada ya kucheza soka maridadi ambalo lilimvutia kila mmoja aliyekuwa anatazama mchezo huo.

Alipata nafasi ya kuanza katika kikosi cha Yanga dhidi ya Rayon Sports, lakini alionekana kutokuwa fiti kwa asilimia 100, ingawaje alikuwa makini katika uchezaji wake.

Kamusoko, ambaye alikuwa anacheza kama kiungo mkabaji katika mchezo huo, licha ya kuwa mzito katika kupeleka mashambulizi, alikuwa na mchango mkubwa wa kukaa na mpira na kuhakikisha anasambaza kwa uhakika.

Wakati benchi la ufundi linafanya mabadiliko ya kumtoa Kamusoko na kumwingiza Rafael Daud, mashabiki walionekana kuchukizwa na kuanza kuzomea uwanjani hapo.

MASHABIKI WAPEWA UHURU

Hii inawezekana iliwasaidia hata Yanga kupata sare juzi. Kwa sababu uhuru ambao walipewa mashabiki wa Yanga kusogea karibu na lango la wachezaji kuingia kwenda uwanjani, kulisaidia kuwapa morali wachezaji wa Yanga.

Kabla mchezo haujaanza mashabiki wa Rayon Sports, walikuwa wamekaa karibu na lango wachezaji kuingia uwanjani, walionekana kabisa kuteka uwanja wote kwa staili yao ya ushangiliaji kwa kutumia ngoma kubwa ambayo walikuja nayo kutoka Rwanda.

Vigogo wa Yanga walionekana kuzungumza kwa dakika kadhaa kisha wote kwa pamoja waliamua mashabiki wao ambao walikaa mbali kusogezwa, hali ambayo iliamsha hamasa uwanjani hapo.