Barcelona yatwaa ubingwa wa Super Cup

Barcelona imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Super Cup, baada ya kuifunga Sevilla kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa nchini Morroco.

Katika mchezo huo Sevilla ndiyo iliyoanza kuzifumania nyavu za wapinzani wao baada ya Pablo Sarabia kuifungia bao la kuongoza katika dakika ya tisa ya mchezo huo.

Beki wa Barcelona, Gerald Pique, aliisawazishia timu yake bao katika dakika ya 42 ya mchezo na timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Katika dakika ya 78 winga wa Kifaransa Ousmane Dembele, aliwainua vitini mashabiki mashabiki wa timu hiyo baada ya kuifungia timu hiyo bao la ushindi.

Kipa wa Barcelona Marc-Andre ter Stegen, ndiye aliyeibuka shujaa katika mchezo huo kwa kuokoa mkwaju wa penati wa dakika za lala salama iliyopigwa na Wissam Ben Yedder.

Barcelona wamecheza michezo tisa kati ya kumi ya Super Cup, lakini huu ukiwa mchezo wa kwanza kwa bingwa kupatikana kwa kuchezwa mchezo mmoja badala ya michezo miwili wa nyumbani na ugenini.

Aidha hii ni mara ya kwanza kwa mchezo wa fainali ya Super Cup kuchezwa nje ya nchi ya Hispania.