Bao larudisha tabasamu la Mo Ibrahim Simba

Muktasari:

Kiungo huyo ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha Simba

Dar es Salaam. Kiungo wa Simba, Ibrahim Mohamed ameanza kurejesha kiwango chake baada ya kufunga bao mmoja katika ushindi wa mabao 4-2 katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussem alimpa nafasi Mo Ibrahim ambaye chini ya Joseph Omog alikuwa anachomeshwa mahindi pale Msimbazi na kugeuka kuwa shuhuda wa kazi za wenzake wakiwa wanacheza.

Mo Ibrahim amelizungumzia hilo kwamba linampa imani kwamba huenda msimu huu ukawa bora zaidi kwake, akiamini anauwezo wa kufanya kazi inayoweza kuleta tija kwa klabu yake.

"Unajua nini hapa kinachotakiwa ni kazi ya kufikisha malengo ya klabu, kazi yangu ni kucheza na si hivyo tu mpira upo damuni kwangu, najipanga kuhakikisha nafasi ninayopewa sitamwangushi kocha.

"Ndani ya timu kuna ushindani wa hali ya juu, lakini ndio unaomfanya mchezaji kujituma kwa bidii ili kazi yake iendelee kuwa bora zaidi na pia itakuwa rahisi kufikia malengo ya kutetea ubingwa," alisema Mo Ibrahim.