Bao la Messi laleta tetemeko la ardhi Barcelona

Muktasari:

Wanasayansi wanasema kila mshambuliaji huyo anapofunga na mashabiki kushangilia kusababisha tetemeko katika jiji hilo

Barcelona, Hispania. Unaweza ukabisha lakini ndiyo ukweli huo, kila Lionel Messi anapofunga jiji la Barcelona hupata tetemeko la ardhi.

Wanasayansi waliweka vifaa vya kupima tetemeko la ardhi kwenye Uwanja wa Camp Nou na kufanikiwa kupima mitetemeko ya ardhi kila nyota huyo wa Barcelona anapofunga.

Athari ya mabao yake huonekana katika data kila wakati mashabiki wanaposheherekea kwa kuruka juu na chini uwanjani hapo.

Vipimo hivyo vilidhihirika wakati Barcelona ilipofanya miujiza ya kutoka nyuma na kuishinda klabu ya Paris Saint Germain katika mtoano wa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Huku wakiwa nyuma kwa mabao 4-0 waliyofungwa katika mchezo wa kwanza na PSG, katika mchezo wa marudiano Barca ilifunga bao la dakika za lala salama na kupata ushindi wa jumla ya 6-5 nyumbani.

Tetemeko la ardhi linalosababishwa na kandanda limejadiliwa katika kongamano la sayansi la Ulaya mji wa Vienna Austria.

Ni kazi ya Jordi Diaz na wenzake katika taasisi ya sayansi ya ardhini iliopo katika mji mkuu wa Catalonia.

Kile ambacho Diaz amegundua ni tofauti iliopo kati ya mashabiki wa soka na wale wa muziki.

Uwanja wa Nou Camp pia huandaa matamasha ya muziki kwa mfano Bruce "The Boss" Springsteen alicheza muziki wake katika uwanja huo 2016.

Kipimo hicho cha Diaz kimewekwa mita 500 kutoka uwanja huo. Kwanza mradi huo wa vipimo ulianza kama mpango wa kuhamasisha kitu cha kuwafanya mashabiki kufurahia kuhusu tawi hilo la sayansi .

Lakini kundi hilo la utafiti lilianza kubaini masuala kadhaa ya kushangaza ambayo yalihitaji uchunguzi.