Banda: Ndondo? Acha kabisa

Muktasari:

  • Imezoeleka kuwaona baadhi ya nyota wa Ligi Kuu Bara wakicheza ndondo mitaani, lakini kwa Banda alipita boda na kutokea Kenya ambako alikwenda kwa kazi hiyo.

USICHOKIJUA kuhusu beki wa Taifa Stars, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini ni kuwa, jamaa kashapiga sana ndondo wakati akichipukia hadi sasa akiwa anatamba kimataifa.

Imezoeleka kuwaona baadhi ya nyota wa Ligi Kuu Bara wakicheza ndondo mitaani, lakini kwa Banda alipita boda na kutokea Kenya ambako alikwenda kwa kazi hiyo.

“Kabla ya kujiunga na Coastal Union, nilianza kucheza soka la mtaani kama kawaida ya wachezaji wengi wa Kitanzania, ambao tunatokea kwenye familia za kawaida.

“Nakumbuka katika mazingira hayo, pia nilikuwa nasoma sekondari tayari nilianza kutegemewa nyumbani, huo ndiyo ukawa mwanzo wa kupiga ndondo pale, Tanga na mwishowe nikawa napata madili ya hadi Kenya,” alisema Banda.

Banda ambaye kwa sasa anatamba na Baroka ya Ligi Kuu Afrika Kusini anadai Abdul Bosnia amehusika kumtoa kwenye aina hiyo ya soka na kuanza kutafuta mafanikio kwenye soka la mfumo rasmi.

“Ndondo ni mpira wa hatari, lakini ilibidi mtu ucheze ili upate kipato, Bosnia nilianza naye kutoka ziro mpaka leo hii nimekuwa moja ya wachezaji muhimu kwa Taifa langu,” alisema beki huyo wa zamani wa Simba.