Balaa la sumu ya Pogba Man united

Muktasari:

Kila mtu anamshangaa kiungo huyo kwa kiwango chake cha siku za karibuni na anavyokalishwa benchi na kinda Scott McTominay.

MANCHESTER, ENGLAND. NDICHO kinachoaminika kwa sasa, kama Jose Mourinho akiendelea kubaki Manchester United basi kuna baadhi ya mastaa akiwamo kiungo Paul Pogba safari ya kuondoka Old Trafford itawahusu.

Kila mtu anamshangaa kiungo huyo kwa kiwango chake cha siku za karibuni na anavyokalishwa benchi na kinda Scott McTominay.

Kiungo Nemanja Matic amewaambia wachezaji wenzake kumwelewa Jose Mourinho anapowashambulia kwa maneno kwa sababu anachokitaka ni mafanikio ya timu nzima na si yake binafsi.

Pogba ameripotiwa kutibuana na Mourinho juu ya kiwango chake cha hivi karibuni, jambo ambalo limemfanya awe benchi kwenye mechi kadhaa kitu na mastaa wa zamani wa soka kumshambulia kwa maneno makali na kusema anastahili kusugua benchi kutokana na soka lake la kivivu analocheza, hasa wengi wakiitaja ile mechi dhidi ya Sevilla, alicheza kwa kiwango cha chini kupita kiasi.

Mesut Ozil, ambaye alishawahi kuwa chini ya Mourinho amesema kocha huyo anapomsema mchezaji hadharani hana nia mbaya, anafanya hivyo kuwavuruga waandishi wa habari ili kukiacha kikosi chake kijiandae kwa mchezo unaofuata bila presha.

Ozil aliandika kwenye kitabu chake kilichofahamika kwa jina la ‘Gunning for Greatness: My Life’, akisema: “Mourinho huwa anafahamu mapema tu kinachokwenda kuandikwa kwenye magazeti, hivyo hufanya kile anachokifanya kwa makusudi ya kuvuruga tu mawazo yao, ambayo kimsingi yangeandikwa basi yangeharibu kabisa morali nzima ya timu.”

Pogba amekuwa gumzo kwa soka lake la kichovu na hilo limemfanya staa zamani wa Ufaransa, Emmanuel Petit, akimwambia Mfaransa mwenzake huyo kuwa acheze mpira na aache kuyachukulia maneno anayosemwa na kocha Mourinho kama ni ugomvi binafsi. Kiungo wa zamani wa Man United, Paul Ince alisema: “Mchezaji ambaye sijawahi kumkosoa ni Pogba, nilidhani anafanywa tu mbuzi wa kafara, lakini kwa kiwango kile alichokicheza dhidi ya Sevilla, nimeanza kuelewa kwa nini wachambuzi wengi wanamkosoa na kocha anamweka benchi. Hovyo kabisa.”

Frank Lampard alisema: “Unapolipa Pauni 90 milioni, unahitaji matokeo, lakini yeye hakuna anachokifanya, kijana, lakini hana uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo.”

Wakati hao yakisemwa na mastaa hao, Gary Lineker alisema kitu kimoja tu, Pogba ni mchezaji anayekuzwa tofauti na uwezo aliokuwa nao. Staa Pogba aliyenaswa kutoka Juventus, anaonekana kulalamika kuhusu nafasi anayochezeshwa, lakini Roy Keane anasema hivi: “Unapokuwa kiungo, unapaswa kuwa na uwezo kucheza ama iwe na wachezaji wawili au watatu. Anapaswa kutuliza akili yake acheze mpira.”

Gary Neville naye alisema yake kuhusu Pogba: “Hajafikia uwezo wa kihivyo, anavyotaka kucheza ni kama soka la kwenda bustani na marafiki. Anataka kucheza kama anapiga video za kuposti kwenye YouTube au Facebook.”

Pogba anaonekana kama kuwa na bifu na Mourinho, ambalo mwisho wake linaweza kumfanya akauzwa tu kwa sababu bosi wa Man United, Ed Woodward, ameshaweka bayana wachezaji wote wanapaswa kutii na kufuata maelekezo ya kocha, yeyote atakayeonekana kupinga, basi safari ya kuondoka Old Trafford itamhusu. Pogba kwanza alianza kulalamikia ujio wa Alexis Sanchez, unamfanya acheze nafasi ambayo hawezi kuimudu, lakini wachambuzi wa masuala ya soka wanaamini mchezaji mahiri, anacheza na kuleta matunda eneo lolote lile alalopangwa, kama inavyotokea kwa mastaa kama Ander Herrera na Ashley Young wanaopafomu kwenye nafasi ambazo hazikuwa zao kimsingi.

Kutokana na hilo, Kocha Mourinho ameonekana tayari anajiandaa na chochote kitakachotokea kuhusu Pogba kwa kubainisha viungo wa kati anaowataka kwenye dirisha lijalo la usajili kuja kuchukua nafasi ya staa huyo.

Viungo hao ni Sergej Milinkovic-Savic wa Lazio, Jorginho wa Napoli, Jean Seri wa Nice, Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur, Toni Kroos wa Real Madrid na McTominay, ambaye anamfanya Pogba kusugua benchi kwa sasa huko Old Trafford baada ya kuonekana pacha mzuri wa Matic sehemu hiyo ya kiungo.

Mourinho amedai Man United inahitaji kuwekeza kwa wachezaji wapya kuifanya timu hiyo kutisha ili hata kocha mwingine atakayekuja kurithi mikoba yake, basi akutane na kikosi kilichosheheni mastaa wa maana tofauti na ilivyokea kwa upande wake ambao kwa sasa anaanza moja kuwasuka wachezaji wake. Kuhusu Pogba kubaki Man United ni suala la kusubiri kuona kitakachotokea baada ya wakala wake Mino Raiola kuripotiwa kuanza kutafuta klabu zinazoweza kumsajili staa huyo anayelipwa Pauni 290,000 kwa wiki huko Old Trafford.