Bajeti ya Dude weka mbali na watoto

Muktasari:

Dude anasema bajeti yake kubwa huenda kwenye mafuta ya gari lakini ukichanganya na msosi na vocha lazima Sh41,000 iteketee kwa siku moja.

UMEWAHI kujiuliza mastaa wa Bongo wanaishije kwa siku? Sasa mkali wa Filamu Bongo, Kulwa kikumba ‘Dude’ matumizi yake ya siku ni zaidi ya mshahara wa msomi wa chuo kikuu mwenye digrii (shahada).

Dude anasema bajeti yake kubwa huenda kwenye mafuta ya gari lakini ukichanganya na msosi na vocha lazima Sh41,000 iteketee kwa siku moja.

“Matumizi yangu ni ya kawaida mno, chai yangu inagharimu Sh3000 tu, chai ya kawaida ya rangi yenye vitafunwa kama mihogo ya kuchemsha, mandazi na vitumbua kidogo.

Mafuta ya gari kwa mzunguuko wa gari yangu hutumia ni Sh20,000 tu kwa siku, kama nitatoka na gari yangu aina ya Mark II Grande, inakula sana mafuta,” anasema Dude ambaye alijizolea umaarufu mkubwa wakati huo akicheza kipindi cha Bongo Dar es Salaam.

“Chakula cha mchana natumia Sh5,000 tu, mara nyingi ugali maharage, samaki kidogo na mboga mboga. Napendelea ugali kwani asili yangu huko unyamwezini huwa ninakula ugali hata asubuhi.

Kwa siku nakunywamaji lita nne (4), nikitoka hununua lita tatu ambayo ni sawa na Sh3,000 lita 1 ya mwisho hunywa nyumbani kabla sijalala,” alisema na kuongeza. “Vocha na matumizi ya simu kwa siku ni Sh5,000. Simu yangu ndiyo ofisi yangu hivyo inatumika mno kwenye utafutaji pesa, kuongea na kuchati kwenye Internet.

Chakula changu cha usiku huwa cha kawaida mno, hakizidi Sh5,000 na mara nyingi huwa wali samaki na mboga mboga hivi, au ndizi nyama na matunda kidogo au glasi ya juice,” alisema.