Babu wa miaka 91 aeleza utamu wa riadha

Muktasari:

  • Aeleza kuwa pamoja na riadha na michezo kuwa ajira lakini kwa upande wake anasisitiza ni zaidi ya ajira kwa kuwa mwili wa binadamu huimalika kwa kufanya mazoezi.

Mchezo wa Riadha umekuwa ukiwavutia watu wengi kushiriki na Joram Zacharia Mollel “Babu” mwenye umri wa miaka 91 ameeleza faida kubwa anavuna kupitia mchezo huo tangu alipoanza kushiriki.

Babu ambaye alizaliwa mwaka 1927 mkoani Arusha eneo la Kijenge Mwaka huu katika mashindano ya Kili Marathon yaliyofanyika Machi 4 Mkoani Kilimanjaro aliweza kushiriki ikiwa ni mara ya 11 tangu aanze kushiriki mashindano hayo mwaka 2007.

“Binadamu anapofanya mazoezi huuweka mwili wake fiti kuliko yule ambaye hafanyi na hili nililiona kwangu maana nisipofanya mazoezi nahisi kuumwa na nikifanya napona na kupitia mazoezi ninajiepusha na maradhi mengi kunishambulia kutokana na uzee wangu,” alisema Mollel.

Pia anaeleza kuhama makazi yake mara kwa mara kulipelekea kupoteza picha zake nyingi, historia ambayo anakosa ukumbusho wake, juhudi daima, Babu anasonga mbele na kujulisha ni jinsi gani riadha kuwa ni sehemu ya maisha yake, sio tu kujipa nguvu kwa kupitia riadha bali nguvu inayomsaidia kufanya shughuli zake za kila siku.

“Mke wa kwanza niliyemchumbia nilimpoenda sana japo walininyang’anya na kati ya wanawake niliyempenda yule wa kwanza ndiye alikuwa kipenzi changu maana nilitumia kila kitu ili nimpate lakini sikudumu naye kwa kuwa nilikuwa naishi mbali naye.”

Babu anasema kuwa hakufanikiwa kumaliza shule kwani aliishia darasa la pili kutokana na kutojua umuhimu wa elimu akiwa anasoma Shule ya Kimandoru mwaka ambao hakuweza kukumbuka mwaka alivyoanza shule.

“Licha ya kufaulu darasa la pili na kutakiwa kuendelea na masomo ya darasa la tatu bado sikupenda shule kutokana na makundi ya ujana pamoja na kuwa na umri mkubwa lakini wenzangu waliosoma walifanikiwa kufika mbali.”

Babu hajafanikiwa kupata mtoto hata mmoja licha ya kuishi na wake watatu kwa nyakati tofauti bado wote hao hakufanikiwa kupata naye watoto kutokana na shughuli zake za ujana zilikuwa zinamuweka mbali nao.

Ameeleza kuwa pamoja na riadha na michezo kuwa ajira lakini kwa upande wake anasisitiza ni zaidi ya ajira kwa kuwa mwili wa binadamu huimalika kwa kufanya mazoezi ambayo kwake ameona faida nyingi kwa kufanya mazoezi.