BOCCO-Simba hii haipoi

Muktasari:

  • Mchezaji bora wa mwezi machi Adam Salamba ndio aliifungia Lipuli bao la kuongoza kipindi cha kwanza dakika ya 31, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’ kabla ya Simba kusawazisha kipindi cha pili.

VINARA wa Ligi Kuu Bara Simba jana walicheza mechi ya 25, dhidi ya Lipuli katika Uwanja wa Samora Iringa na mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, na vinara hao kutimiza pointi 59.

Mchezaji bora wa mwezi machi Adam Salamba ndio aliifungia Lipuli bao la kuongoza kipindi cha kwanza dakika ya 31, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’ kabla ya Simba kusawazisha kipindi cha pili.

Simba waliingia kipindi cha pili wakiwa nyuma na dakika ya 45, walifanya mabadiliko kwa kumtoa beki Juuko Murshid na kuingia Laudit Mavugo ambaye alikuja kufunga goli dakika ya 66, baada ya kupokea mpira wa kona kutoka kwa Shomary Kapombe ambao ulikuwa piga nikupige.

Baada ya matokeo hayo Simba wanaongeza ushindani katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu kama watani zao Yanga ambao wanashika nafasi ya pili watashinda mechi zao tatu za viporo.

Simba baada ya sare dhidi ya Lipuli mechi ambayo inafaata itakuwa dhidi ya Yanga ambayo itachezwa Aprili 29, na hiyo ndio inaweza kutoa taswira kama watashinda wanaweza kuchukua ubingwa, lakini wakipoteza au sare ubingwa utakuwa bado upo wazi.

Kwa maana hiyo mechi ya vinara Simba walikuwa na pointi 59, dhidi ya watani zao Yanga ambao wanacheza leo dhidi ya Mbeya City kama wakishinda nao watakuwa na pointi 50, huku wakiwa na viporo viwili inaweza kutoa taswira ya ubingwa msimu huu.

Matokeo haya ya Simba dhidi ya Lipuli yatakuwa yameongeza pia presha kwa Simba katika mechi tano ambazo wamebaki nazo na ikiwemo dhidi ya Yanga na hakuna ambayo anatakiwa kupoteza au hata sare ili kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Nahodha wa Simba John Bocco alisema matokeo dhidi ya Lipuli hayakuwa malengo yao kwani, walitamani kutoka katika mechi hiyo wakiwa na pointi tatu, lakini hata pointi moja ya ugenini si mbaya.

Bocco alisema ligi ni ngumu na ubingwa bado unaonekana bado upo wazi, lakini watahakikisha wanarekebisha makosa waliyoyafanya kwenye mechi dhidi ya Lipuli ili kushinda mechi ijayo dhidi ya Yanga na kuongeza pointi.

“Lipuli walikuwa vizuri katika mechi ya leo na ni miongoni mwa timu nzuri ambazo zimetupa shida msimu huu kuzifunga kwani, hata mechi ya kwanza ilimalizika kwa matokeo haya lakini nina imani benchi la ufundi limeona upungufu na wachezaji watakwenda kuyafanyia kazi,” alisema.

“Malengo yetu ni kuchukua ubingwa ili kufanya hivyo ni kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi zetu zote tano ambazo tumebaki nazo bila kujali tunacheza nyumbani au ugenini na kufikia malengo ambayi tumejiwekea msimu huu,” alisema Bocco.

“Ligi ni ngumu kila timu imejipanga hata wapinzani wetu ambao wapo katika nafasi ya pili na tunakimbizana nao katika mbio za ubingwa nao wanaweza kuteleza katika mechi yoyote kama ilivyokuwa kwetu,” aliongezea Bocco.

Kocha wa Lipuli Selemani Matola alisema matokeo ya mechi mbili dhidi ya Simba ule wa mzunguko wa kwanza ambao nao ulimalizika kwa sare ya 1-1, umemfurahisha na kuondoa maneno ya kuonekana wanauswahiba na timu hiyo.

“Mara zote tunaonekana Lipuli tuna ukaribu na Simba na tunaonekana tunaweza kucheza chini ya kiwango lakini matokeo yamejidhihirisha sivyo.”