Azam yazitaka pointi tatu za Mwadui leo

Muktasari:

Azam haijawahi kufungwa na Mwadui katika michezo mitatu waliyocheza Mwadui

Dar es Salaam. Azam inaikabili Mwadui FC leo Ijumaa ikitafuta pointi tatu ili kuishusha Mbao kileleni lakini  itamkosa mshambuliaji wake Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu na beki  Abdallah Kheri.

Kutinyu alikwenda kwao Zimbambwe kuitumikia timu ya Taifa na bado hajarejea wakati Kheri ni majeruhi.

Azam iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita baada ya kucheza michezo miwili na kushinda yote dhidi ya Mbeya City kwa mabao 2-0 na Ndanda kwa mabao 3-0.

Kocha Mkuu wa Azam, Hans Van Der Pluijm amesema wachezaji wake wanatakiwa kujiamini wenyewe ili kupata ushindi katika mchezo huo utakoanza saa 8:00 mchana.

 “Nimekiandaa vizuri kikosi changu kuelekea mchezo huo na naamini kuwa tutapata matokeo mazuri ingawa mimi kujiamini si jambo la kujipa uhakika bali wachezaji wanatakiwa kujiamini wenyewe kuwa wanaweza kupata matokeo mazuri ugenini," alisema Pluijm.

 Azam inapambana na Mwadui ikiwa na rekodi bora dhidi ya timu hiyo ya Kanda ya Ziwa kwani zimekutana mara sita katika michezo wa Ligi Kuu Bara huku Azam ikishinda mara tano na sare moja.

Kwenye Uwanja huo wa Mwadui Complex timu hizo zimekutana mara tatu na Azam ikishinda mara mbili na kupata sare moja.

Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kushinda mchezo huo licha ya kukiri utakuwa mgumu kwani Azam ni moja ya timu nzuri.