Azam yaibana Yanga kila kona

Muktasari:

  • Yanga ipo nafasi ya tatu na pointi 48 hivyo inatakiwa kushinda mchezo wa leo ili kupunguza tofauti ya pointi baina yake na Azam kuwa nne. Azam ina pointi 55 katika nafasi ya pili. Endapo Yanga itashindwa kupata ushindi dhidi ya Mbao ni rasmi kuwa itamaliza ligi katika nafasi ya tatu kwani haitaweza kuzifikia pointi za Azam FC tena.

MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga leo Jumanne watapambana na hali yao dhidi ya Mbao FC ya Mwanza katika mchezo ambao utaamua hatma yao ya kumaliza katika nafasi mbili za juu msimu huu.

Yanga ipo nafasi ya tatu na pointi 48 hivyo inatakiwa kushinda mchezo wa leo ili kupunguza tofauti ya pointi baina yake na Azam kuwa nne. Azam ina pointi 55 katika nafasi ya pili. Endapo Yanga itashindwa kupata ushindi dhidi ya Mbao ni rasmi kuwa itamaliza ligi katika nafasi ya tatu kwani haitaweza kuzifikia pointi za Azam FC tena.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa mtego kwa Yanga kama itavunja mwiko wa kutoshinda katika mechi tisa mfululizo katika mashindano yote.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu mechi zake tisa za mwisho walicheza na Singida United ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, wakafungwa 1- 0 na Welaitta Dicha 1-0, wakafungwa na Simba 1-0, Tanzania Prison 2-0, Mtibwa Sugar 1-0, Mwadui 1-0, USM Alger 4-0 walitoka sare katika mechi kati ya Mbeya City 1-1, Rayon Sport 0-0. Yanga inaingia kwenye mechi hiyo dhidi ya Mbao FC ikiwa na kumbukumu mbaya ya kupoteza michezo mitatu iliyocheza na wababe hao wa soka jijini Mwanza. Kocha wa Mbao FC, Fulgence Novatus alisema mechi ya leo watacheza kwa kushindana ili kuendeleza kiwango chao ambacho wamekuwa wakionesha kila wanapocheza na Yanga haswa wakiwa katika uwanja wa CCM Kirumba. “Kwanza tutacheza bila ya kuwa na presha yoyote kwani tumeshakuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu, kwahiyo tutacheza vizuri na tutakuwa na wakati mzuri wa kushinda na itakuwa faida kwa wachezaji kucheza kwa kiwango cha juu ili kuonekana na timu kubwa,” alisema Novatus.