Azam wazindua redio yao

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Azam Media, Tido Muhando alisema redio yao itatambulika kwa jina la (U FM) ambayo itapatikana kwa masafa ya 107.3 ikiwa na kauli mbio ya (Sisi ni wewe) ambayo itaanza kufanya kazi kwanza hapa Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kampuni ya Azam Media Group ni wadhamini wenye haki ya kuonyesha matangazo ya Ligi Kuu Bara leo Ijumaa rasmi walitangaza kuzindia redio yao iliyokuwa katika majaribio kwa miaka miwili iliyopita.
Mkurugenzi wa Azam Media, Tido Muhando alisema redio yao itatambulika kwa jina la (U FM) ambayo itapatikana kwa masafa ya 107.3 ikiwa na kauli mbio ya (Sisi ni wewe) ambayo itaanza kufanya kazi kwanza hapa Dar es Salaam.
Muhando alisema wamejipanga kuhakikisha inakuwa redio ya tofauti kulinga na ambazo zinasikika hapa nchini kwa sasa kwani watakuwa wanawapa watu taarifa kwa haraka zaidi tena zenye uhakika.
"Tutaweka maudhui yote ambazo watu wa umri mbalimbali akisikiliza redio yetu atakuwa hatamani kubadilisha kwani kila kitu kitakuwa kinapatikana hapo kwa nyakati tofauti tukiwa na leo lengo la kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha," alisema Muhando.
"Tupo tayari kujitofautisha na redio zote tumejipanga katika kutafuta habari zenye uhakika katika nyanja zote na kuwapatia wasikilizaji wetu muda wote na siku si nyingi tutaanza kusikika mpaka mikoani kwani kuna vibali tunavisubili," alisema Mkurugenzi wa michezo wa Azam Media, Baruani Muhunza.
"Tutaanza kusaka vipaji vya kuimba muziki na washindi watakaopatikana tutawapeleka studio kwa Man Water ili kurekodi nyimbo zao, lakini tutakuwa na vipindi vingine vingi nje ya studio," alisema Meneja wa redio Wasiwasi Mwabulambo.