Azam wakikupiga bao, sahau kurudisha

Muktasari:

Kabla ya mechi ya Lipuli jana Jumapili usiku, Azam ilikuwa haijaruhusu bao hata moja.

AZAM imeimarisha safu yake ya ulinzi vilivyo chini ya mabeki Daniel Amoah, Yakubu Mohammed na Aggrey Morris na sasa imedai pindi wanapopata bao moja wanakuwa na uhakika wa ushindi kwani ili timu pinzani iwafunge ni lazima itoe jasho.

Nahodha wa Azam, Himid Mao alisema kwa sasa wanafanya kazi kubwa kuhakikisha hawaruhusu bao ili ikitokea tu wamefunga hata bao moja waweze kuondoka na pointi zote tatu. Kabla ya mechi ya Lipuli jana Jumapili usiku, Azam ilikuwa haijaruhusu bao hata moja.

Mao ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Pamba na Mtibwa Sugar, Mao Mkami alisema safu hiyo inafanya kazi kubwa na inacheza kwa uelewano kitendo kinachowapa uhakika wa kuondoka na pointi uwanjani.

“Unajua timu ikishakuwa na safu nzuri ya ulinzi mnakuwa na uhakika wa angalau pointi moja, mnachofanya ni kutafuta bao ili mpate pointi zote tatu. Tukipata nafasi tutafunga mabao zaidi,” alisema.

Akizungumzia ratiba ya mechi tatu za ugenini wanazokwenda kucheza kuanzia wikiendi hii, Mao alisema watakabiliana na changamoto nyingi lakini wana uhakika kuwa watapata pointi. Azam baada ya kumalizana na Lipuli jana Jumapili, itakwenda ugenini kucheza na Singida United, Mbao FC na Mwadui.

“Mechi za ugenini ni ngumu sana, hata hivyo hiyo siyo sababu ya kuogopa. Tunakwenda kupambana,” alisema.