Azam waitambia URA kwa rekodi

Muktasari:

Azam ilipokuwa inajiandaa na ligi kuu ilikwenda Uganda na kucheza mechi tano za kirafiki, katika michezo hiyo hawakupoteza hata mmoja hivyo rekodi hiyo itawabeba.

KLABU ya Azam FC itaiwakilisha Tanzania katika fainali ya Kombe la Mapinduzi hapo kesho Jumamosi itakapocheza na URA ya Uganda , lakini uongozi wa klabu hiyo umetamba kushinda kutokana na kuwa na rekodi nzuri kwenye mashindano hayo kila wanapokutana na timu hiyo, inayomilikiwa na mamlaka ya mapato ya nchi hiyo.

Meneja wa Azam,  Philip Alando, anasema walipokuwa wanajiandaa na ligi walienda Uganda na kucheza mechi tano, katika michezo hiyo hawakupoteza hata mmoja hivyo rekodi hiyo itawabeba .

“Tulienda Uganda tukacheza mechi za kirafiki kule, katika mechi tano tulizocheza hatukupoteza hata moja. Tulicheza na hawa URA tukawafunga mabo 2-0, kwa hiyo hata mchezo huu nina imani tutafanya vizuri ,” anasema.

Alando anaongeza na kusema, wanataka kuchukua kombehili ili iwe maraya pili mfululizo: “Hii itakuwa historia kwetu katika kombe hili na kuitengenezea sifa nchi yetu pia katika kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania dhidi ya timu za Uganda”.

“Timu za Uganda hazitusumbui sisi lakini tunawaheshimu kwa namna moja ama nyingine, wasitegemee wepesi katika mchezo huu kwa sababu tunataka tuchukue kombe kwa mara ya pili,” anasema Alando.