Azam lazima kieleweke leo

Saturday January 13 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN, UNGUJA

WATETEZI wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam leo Jumamosi watakuwa na kibarua kigumu wakati watakapowakabili kwa mara nyingine URA ya Uganda katika mchezo wa fainali, huku matajiri hao wakitamba lazima kieleweke.

Azam katika mechi yao ya makundi dhidi ya wababe hao wa Uganda walilala bao 1-0, lakini katika mechi ya leo Kocha wa timu hiyo ameapa kuwa, hawatakubali tena kufungwa kwa sababu wanataka kuweka rekodi ya kulibeba taji kwa mara ya nne. Kocha Aristica Cioaba alisema mechi dhidi ya URA ni ngumu kwao haswa wakiwa wameshapoteza mechi ya kwanza dhidi yao, lakini watawavaa kivingine leo Amaan.

“URA ni timu nzuri, wanashambulia wachezaji wote na kukaba wote, yaani inacheza kitimu zaidi. Ila tumejipanga hawatufungi kwa mara ya pili,” alisema.

Kocha wa URA, Nkata Paul alisema wakati wanaanza mashindano walikuwa wakicheza kawaida kutokana na uchovu wa safari lakini sasa wako fiti.

“Tumeshindwa kufunga magoli mapema na haraka kwani kuna washambuliaji wetu watatu tegemezi tumewaacha ila tumejipanga tunashinda,” alisema.

Kama Azam ataibuka mshindi kwenye mchezo huo, atakuwa amebeba taji hilo kwa mara ya nne.